CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Kanda ya Mashariki, imetoa onyo kwa madereva ambao hawajapata mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali na wamekuwa wakitumia vyeti vya madereva waliopata mafunzo kusafirisha kemikali kuacha mara moja tabia hiyo, la sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Onyo hilo limetolewa leo na Meneja wa Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa madereva wanaosafirisha kemikali ndani na nje ya nchi yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa FPTC –Kurasini Jijini Dar Es Salaam.

Mkapa amesema wamebaini baadhi ya madereva na kampuni za usafirishaji wa kemikali wameshindwa kuwa waaminifu, kwani wamekuwa wakiwatumia madereva waliopatiwa mafunzo kupakia kemikali lakini linapokuja suala la usafirishaji wamekuwa wakiwatumia madereva ambao hawajapata mafunzo kutoka Mamlaka, kitendo ambacho ni uvunjifu wa sheria.

“tumebaini kwa sasa baadhi ya madereva mmeanza kutumia uhuru wenu vibaya, tumegundua kuna baadhi yenu wakati wa kupakia mizigo ya kemikali anakuwepo dereva mwenye cheti na aliyepatiwa mafunzo lakini wakati wa kusafiri anasafiri ambaye hajapata mafunzo, naomba tuache hii tabia mara moja.” Alisema Mkapa.

Aidha, Mkapa amesema watafanya ukaguzi ili kujiridhisha kama ni kweli kitendo hicho kinafanyika na endapo kuna madereva watabainika kufanya hivyo basi watachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake Mkemia kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Leonora Kombo, amewataka madereva hao kufanya kazi zao kwa weledi na kuepuka kushirikishi kwenye uchepushaji wa kemikali bashirifu ambazo zinaweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya.

“Tunawakumbusha kuzingatia weledi na kuepuka kushiriki kwenye uchepushaji wa kemikali, mkumbuke kemikali hizi zikitumika vibaya madhara yake ni makubwa kwa jamii na hata kwa taifa. Endapo utabainika kufanya hivi utachukuliwa hatua kali kisheria, hivyo nawaomba msifanye hivyo.” alisema Leonora

Akizungumza kwa niaba ya Madereva waliopatiwa mafunzo, Dereva wa kampuni ya JIREMA, Salmin Karugendo, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa jitihada inayochukua katika utoaji wa mafunzo kwa madereva wanaosafirisha kemikali, mafunzo ambayo amesema yatawasaidia kuwaepusha na madhara yanayoweza kuletwa na kemikali pale ambapo ajali zinatokea wakati wa usafirishaji.

Copyright ©2023 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.