Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Februari 4, 2023 imefanya ziara kwenye Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), jijini Dar es Salaam na kutembelea maabara kwa ajili ya kuona shughuli za uchunguzi wa kimaabara zinazotekelezwa na Mamlaka kwa umma.
Akiongea baada ya kutembelea maabara, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Aloyce Kamamba, ameipongeza Mamlaka kwa kazi nzuri inayoifanya ya kiuchunguzi na huduma bora zinazotolewa na kushauri kupanua wigo wa huduma wa wananchi ikiwezekana zipatikane katika kila Mkoa hapa nchini.
“Nawapongeza sana kwa huduma nzuri mnazozitoa ambazo nyingine tulikuwa hatuzifahamu, mnafanya kazi nzuri sana na katika mazingira mengine magumu. Huduma hizi za Mkemia Mkuu wa Serikali zinahitajika sana, wapo watu wengi wanazohitaji hata huduma za DNA. Kwa hiyo tunashauri huduma hizi zisogezwe maeneo wananchi walipo hasa kwenye maeneo ya mikoa na ikiwezekana kuwa na ofisi kila Mkoa ili wananchi waweze kupata huduma zenu kwa urahisi zaidi” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Aloyce Kamamba, imeiagiza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali nchini juu ya matatizo na changamoto kuhusu madhara yatokanayo na sumu kuvu ili nchi iweze kufanya vizuri katika ngazi ya kimataifa katika uuazaji wa mazao ya chakula.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel, akizungumza baada ya Kamati kutembelea maabara za Toksikolojia, Sayansi Jinai Kemia, Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba na maabara ya mitambo, amesema Wajumbe wa Kamati wameridhishwa na utekelezaji wa kazi za Mamlaka.
"Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ufanyaji kazi mzuri katika kuhudumia wananchi kwenye masuala mbalimbali ya kijamii kupitia uchunguzi wa kimaabara unaofanyika kwa umakini mkubwa. Pia Wizara ya Afya ipo tayari kufanyia kazi hoja zilizotolewa na Wajumbe baada ya kukagua Maabara zote kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi," alisema Dkt. Mollel.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea Mamlaka na kujionea shughuli zinazotekelezwa kwa ufanisi kwenye masuala ya uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara wa Sampuli na vielelezo mbalimbali vya kijamii na jinai, vile vile alisema Mamlaka itakwenda kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.