CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefanikiwa kupata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO/IEC 17025:2017 kutoka Southern African Development Community (SADCAS).

Mkemia Mkuu wa Serikali ametoa taarifa hiyo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti cha Mfumo wa Ubora wa Maabara kwa watumishi wa Kurugenzi ya Huduma za Sayansi Jinai kilichofanyika Novemba 8, 2022 katika ukumbi mdogo wa Bunge jijini Dar es Salaam.

“Tumefanikiwa kupata ithibati ya maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba na SADCAS wametujulisha kwa barua pamoja na cheti cha ithibati kimefika na tumekipokea jana, nawapongeza watumishi wote wa Mamlaka waliofanikisha kupatikana kwa ithibati hii kwa sababu haikuwa kazi nyepesi kuipata kwake. Naamini ithibati hii itaongeza chachu ya maabara yetu kuaminika zaidi katika masuala ya uchunguzi wa kimaabara katika masuala ya sayansi jinai na vinasaba” alisema Dkt. Mafumiko.

Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amewataka watumishi wa maabara ya vinasaba kufanyakazi kwa bidii kwa kuzingatia matakwa ya ithibati ili kuilinda na kuishi katika misingi ya mifumo ya ubora.

“Tujikite kwenye matakwa ya ithibati na tuyaishi katika kazi zetu za kila siku za uchunguzi kwa kuzingatia mambo ya muhimu ya utekelezaji wa mifumo ya ubora. Katika kuishi misingi ya mifumo ya ubora inapaswa iwe ni kipaumbele cha mtumishi binafsi na taasisi kwa ujumla ili kila mtumishi uweze kufanyakazi katika maabara yoyote kwa sababu hakuna mtumishi mwenye hati miliki ya kuwa kwenye maabara moja.

Kila mtumishi anapaswa kuwa na uwezo wa kufanyakazi na kuzungumzia maabara zote na huo ndio umahiri unaohitajika. Ithibati hii ya maabara ya Vinasaba ituhamasishe kupata ithibati ya maabara nyingine za Mamlaka ili kutimiza malengo ya kuwa na ithibati ya maabara zetu zote” alisisitiza Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kupatikana kwa ithibati ya maabara ya sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba kufanya sasa Mamlaka kuwa na maabara tatu kati ya saba ambazo zimepata ithibati ya uchunguzi wa kimaabara. Maabara nyingine ni ya mazingira na chakula na dawa.

Kupata ithibati kwa maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba kunaifanya kuwa maabara ya kwanza ya Vinasaba kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na maabara ya nne kwa nchi za Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika. 

Copyright ©2023 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.