Madereva wanaojihusisha na usafirishaji wa kemikali nchini na nje ya nchi, wameeleza kuwa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali yanayotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, yamewasaidia kuwapa uelewa wa tabia za kemikali, kuzingatia taratibu za usafirishaji salama wa kemikali na kuchukua tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kuletwa na kemikali pindi itakapotokea ajali wakati wa usafirishaji.
Hayo yamebainishwa na madereva wa kampuni ya usafirishaji wa kemikali ya Golden Coach, wakati wa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali yaliyotolewa jana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam yakihusisha zaidi ya madereva 36 wa kampuni hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Madereva wa kampuni hiyo, Dereva Isihaka Omary, amesema awali walikuwa hawaelewi chochote kuhusiana na usafirishaji salama wa kemikali zaidi ya kufanya kazi kwa mazoea, lakini baada ya mafunzo hayo wameweza kutambua taratibu na kanuni mbalimbali zinazowaongoza katika usafirishaji wa kemikali, pamoja na namna ya kulinda afya zao pamoja na mazingira.
“Ni wazi kuwa mmetufumbua macho juu ya kufuata taratibu na kanuni zote zinazotuongoza kwenye usafirishaji wa kemikali na tumeweza kuelewa zaidi namna ya kujikinga na madhara ya kemikali endapo ajali inapotokea. Kusema ukweli tunawashukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Mashariki kwa kutupa mafunzo haya. Tunaahidi kwenda kutekeleza yale yote tuliyofundishwa” alisema Isihaka.
Kwa upande wake Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Golden Coach, Chrispin Kayombo, amesema mafunzo hayo yameiwezesha kampuni kuongeza idadi ya madereva wanaoweza kuruhusiwa kusafirisha kemikali ndani ya nchi na nje, na kuiwezesha kampuni hiyo kuweza kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani ya Mwaka 2003.
“Tunaushukuru uongozi wa Mamlaka kwa kutoa muda wao wa siku mbili kuhakikisha madereva wetu wanapata mafunzo haya ya usafirishaji salama wa kemikali na kuwawezesha kuruhusiwa kusafirisha kemikali kama sheria inavyowataka” alisema Chrispin.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, amewataka madereva wa kampuni kufanyia kazi mafunzo hayo kwa kuhakikisha wanachukua tahadhari zote walizofundishwa kuhusiana na usafirishaji salama wa kemikali.
Mkapa amesema kuzingatia kwao kutawezesha kuwaweka salama dhidi ya madhara yanayoweza kuletwa na kemikali na Mamlaka hiyo itaendelea kuwa karibu nao kuhakikisha wanapatiwa zaidi elimu kuhusiana na usafirishaji salama wa kemikali