CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi wametakiwa kupata elimu ya usimamizi na usafirishaji salama wa kemikali hatarishi pamoja na kufuata kanuni na sheria za usafirishaji wa kemikali nchini.

Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, alisema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya madereva 140 wanaosafirisha mizigo ya kemikali yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.

“Wasafirishaji wote wa kemikali hatarishi mnatakiwa kisheria kuwa na vibali vyote Mkemia Mkuu wa Serikali ambavyo vinahitajika wakati wa kusafirisha kemikali na kuhakikisha kemikali inasafirishwa kwa usalama na dereva awe amepitia mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali ili kuondokana na athari pale inapotokea majanga wakati wa usafirishaji wa kemikali,” alisema Elias.

Pia Mkurugenzi alibainisha kuwa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali, yatolewe kwa wamiliki wa magari na makampuni kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya faida ya kuwapeleka madereva na wasimamizi wa kemikali kupata elimu hiyo na kuelewa changamoto zinazowakabili madereva pindi wanaposafirisha kemikali na namna ya kuzitatua.

Aidha, aliwasisitiza madereva kuzingatia kanuni na sheria za usafirishaji wa kemikali hatarishi ili kuepusha kuleta madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, amewasihi madereva kufahamu na kutambua aina ya kemikali wanayosafirisha ili kuweza kuchukua tahadhari kabla na wakati wa kusafirisha kemikali kwani usafirishaji wa kemikali unahitaji umakini mkubwa.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Ali Mhina, dereva kutoka kampuni ya Tazama Pipe Line ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa kutoa mafunzo kwa madereva kwani mafunzo humjenga dereva kwa kujitambua, kuwa makini pamoja na kuitambua jamii.

“Tunaipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutambua umuhimu wa afya na usalama wa dereva na kuhakikisha dereva anasafirisha kemikali kwa usalama, mafunzo haya yatatusaidia katika kusafirisha mizigo ya kemikali kwa usalama mkubwa ukilinganisha na tulivyokuwa tunaifanya kazi hii kabla ya mafunzo haya” alisema Ali.

Copyright ©2022 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.