CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Wananchi wamehimizwa kuendelea kutumia fursa mbadala za kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na tatizo la dawa za kulevya kwani siyo tu zinakwamisha kufikia mifumo endelevu ya chakula bali inakwamisha juhudi za kutokomeza umaskini.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Arusha, Eliamini Mkenga, katika Maonesho ya 29 ya Kilimo ya Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Nanenane Themi-Njiro, Arusha.

Meneja Mkenga, amesema kuwa vijana na wanawake ni tegemezi katika ukuaji wa uchumi wa taifa na mifumo endelevu ya chakula, hivyo waache kujishughulisha na kilimo cha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi na badala yake wafanye kilimo cha halali ambacho kitawaingizia kipato.

“Tumewaletea huduma ya upimaji wa dawa za kulevya inayosaidia kupunguza matumizi yasiyofaa ya dawa za kulevya ambazo husababisha uzalishaji uwe wa chini kutokana na vijana wengi kujiingiza kwenye matumizi ya dawa hizo na hivyo tunasaidiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha kwamba wale ambao wanazalisha, wanasafirisha, wanaouza na watumiaji wanadhibitiwa,” alisema Mkenga.

Aidha, Meneja, ameongeza kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya Maonesho ya 29 ya Kilimo ya Nanenane 2023, inayosema ‘Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula’ Mamlaka itaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya usalama wa chakula katika kuhakikisha wanatumia chakula ambacho ni salama kwa matumizi ya binadamu.

“Kwa kutambua athari zinazoweza kutokea kwa sababu ya ulaji wa chakula kisicho salama kutokana na kuwa na sumu, vimelea na kemikali kuanzia katika hatua ya uzalishaji, uhifadhi na usindikaji, Mamlaka inatoa huduma ya kupima ubora wa mazao na chakula pamoja na kutambua uchafuzi wowote uliofanyika katika mazao hayo kabla ya kutumika, kwa kutumia mitambo ya kisasa kama vile ‘Liquid Chromatography Mass Spectrometer (LC-MS)’ , ‘Gas Chromatography Mass Spectrometer (GC-MS) na Atomic Absorption Mass Spectrometer (AAS-MS), hivyo kuongeza usalama wa chakula,” aliongeza Mkenga.

Sambamba na hilo, Meneja, anawakaribisha wadau wa kemikali na wazalishaji wa vyakula kutembelea ofisi za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili waweze kupata huduma ya usajili na vibali vya kemikali kwa kutumia  mtandao na huduma za kiuchunguzi wa maabara.

Copyright ©2023 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.