Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuongoza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha pili cha miaka mitano.
Dkt. Fidelice Mafumiko, ameyasema hayo wakati akiongea na Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma mara baada ya kuteuliwa Machi 25, 2023.
“Namshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Imani yake kwangu na kuona kwamba ninaweza kwa kushirikiana na wenzangu kuendelea kuitumikia taasisi hii kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Naamini imani aliyoiweka kwetu kupitia mimi ni kubwa kwa sababu mimi peke yangu siwezi kutekeleza majukumu yote. Naamini namna pekee nzuri ya kutimiza imani ya Mheshimiwa Rais ni kufanya kazi kwa kasi, uadilifu na weledi zaidi ili kutimiza matarajio yake kupitia taasisi hii” alisema.
Mkemia Mkuu wa Serikali amewashukuru Watumishi wa Mamlaka kwa upendo na imani waliyoionesha kupitia ujumbe wa pongezi mara baada ya kutangazwa kwa uteuzi wake na kuwataka kuendeleza ushirikiano, upendo na mshikamano kwa maslahi makubwa ya taasisi.
“Watumishi wenzangu upendo wenu nimeupata kwa namna tofauti tofauti baada ya taarifa ya uteuzi wangu kutolewa kupitia ujumbe wenu wa pongezi ambao ndani yake una sala na maombi ambayo yamenifanya nijisikie vizuri napenda kuwashukuru sana. Namshukuru Mungu kwa taasisi yetu kwa ule upendo, ushirikiano na mshikamano ambao unatufanya kuwa familia moja.
Naweza kuwaambia kwamba sisi wote tunategemeana na hakuna kiongozi anayeweza kufanya yote peke yake isipokuwa kuna wakati lazima aoneshe dira kwamba tunaelekea huku. Kazi yangu mimi kama kiongozi wenu ni kuratibu ila wote tunatekeleza. Sisi ndio tutakaofanya taasisi hii iendelee kupewa thamani ile ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipatia’’ alisisitiza.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewasihi watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea na kazi na kudumisha upendo na kusema asitokee mtumishi mmoja akajiona ni bora kuliko mwingine bali wote ni bora kwa sababu ikitokea changamoto au furaha ni ya wote na mwisho wa siku kutambua tumechangia kitu gani katika maendeleo ya taifa.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Evaclotida Kapinga, akiongea kwa niaba ya Watumishi amempongeza Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuteuliwa na kumtakia afya njema katika utekelezaji wa majukumu yake ili kutimiza malengo ya Mamlaka na Serikali kwa ujumla.
“Tunakupongeza kwa kuteuliwa kwa awamu ya pili kutuongoza tena. Tunakutakia afya njema na Mungu aendelee kukulinda na kukuongoza ili uweze kukamilisha majukumu yako ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona bado unaweza kuyasimamia na kusogeza mbele kupitia Mamlaka kwa lengo na manufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alimaliza.