CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka viongozi kufanya maamuzi ya majukumu yanayowahusu badala ya kushauri kila jambo, wakati mambo mengine wanaweza kufanya maamuzi.

Mkemia Mkuu wa Serikali, amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo elekezi ya masuala ya uongozi kwa Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

“Malengo ya mafunzo haya ni kuongeza uwezo katika kutatua changamoto za kiutendaji pale unapoongoza, kupunguza kutegemea kushauri katika kila kitu, hususan kwa masuala ambayo unatakiwa kufanya uamuzi unatakiwa kuamua ili kuwezesha kazi ziendelee na kuongeza uwajibikaji kama kiongozi ni jambo la muhimu. Unapoteuliwa unapewa majukumu na wajibu wako kwa viongozi wa juu na wale wa chini unaowangoza ili kuimarisha mshikamano na ufanisi katika utendaji kazi” alisema.

Aidha, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewaeleza washiriki wa mafunzo kwamba wanatakiwa kutambua uongozi ni kubadilishana vijiti na mtumishi anapopewa uongozi anatakiwa kubeba majukumu yote na kuyatekeleza ipasavyo. Alieleza kuwa ni muhimu kwa kiongozi kufahamu namna bora ya kuwasiliana na viongozi wake wa juu na watumishi anaowaongoza ili kujenga timu inayofanyakazi kwa umoja.

“Kiongozi anapaswa kujua namna ya kuongea na viongozi wake wa juu na watumishi anaowaongoza, kiongozi wako wa juu unamshauri na wa chini yako unamuelekeza kwa kutumia lugha nzuri. Hivyo, unapaswa kujua unawasiliana vipi na viongozi wako na unawasilisha vipi masuala chanya ya Serikali yako, au na wewe ni sehemu ya kulalamika? Unatakiwa kujua namna gani unaweza kuchangamana na viongozi wenzako na watumishi waliopo chini yako wakaona unastahili kuwaongoza na kuishi nao vizuri” alimaliza.

Naye Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo, Magdalena Mtenga, akiongea kwa niaba ya washiriki alimshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa maelekezo aliyoyatoa kupitia hotuba yake na kuahidi kujikita kwenye mafunzo ili kupata uelewa wa kutosha ambao utawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tunashukuru kwa maelekezo uliyotupatia, tutajitahidi kuelewa ipasavyo mafunzo haya ili kuweza kukusaidia katika utekelezaji wa majukumu na kuwezesha malengo ya taasisi kwenda mbele” alimaliza. 

Copyright ©2023 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.