CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

MKEMIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WATUMIAJI WA KEMIKALI YA ZEBAKI KUJISAJILI

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka wadau wa kemikali aina ya zebaki kujisajili na kutambuliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa sababu kemikali hiyo haijazuiwa kutumika nchini.

Mkemia Mkuu wa Serikali amesema hayo jijini Mwanza wakati akiongea na waandishi wa habari na kutambulisha makampuni kumi ambayo yamesajili kisheria kwa ajili ya kuingiza kemikali hizo nchini ambazo zinatumika kwenye migodi kwa ajili ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

“Ifahamike kuwa, Sheria inaagiza kila anayejihusisha na kemikali ikiwemo Zebaki anapaswa kusajiliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye ndiye Msajili wa kemikali za Viwandani na Majumbani hapa nchini. Hadi tarehe 22/08/2022, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inazitambua kampuni kumi ambazo zilikidhi na kutimiza matakwa ya sheria, na hivyo kuzisajili, ambazo kuanzia mwezi Septemba 2021 mpaka sasa zimeweza kuingiza nchini takribani tani tano za kemikali aina ya Zebaki kwa njia inayotambulika kisheria.

Hivyo basi, ninaelekeza wadau wote wanaojihusisha na Zebaki ikiwemo watumiaji ambao hawajasajiliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wafuate taratibu za sheria na kanuni katika ununuzi, uuzaji, utumiaji na usambazaji wa kemikali hiyo” alisema.

Aidha, Dkt. Mafumiko, alisisitiza kwamba Utaratibu wa kuingiza kemikali ya Zebaki kwa kufuata sheria utaiwezesha serikali kusimamia na kudhibiti uingizaji, usambazaji pamoja na utoaji wa elimu matumizi sahihi ya Zebaki nchini ili kulinda afya na mazingira.

Naye Fredrick Otieno kutoka Kampuni ya Jema Chemicals ambayo ni moja ya kampuni zilizosajiliwa kuingiza kemikali ya Zebaki nchini, aliishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuweza kuwasajili na kufanya biashara ya kemikali hiyo kulingana na matakwa ya kisheria, aidha, ameiomba Mamlaka kushirikiana nao kwa pamoja katika kutoa elimu ya matumizi salama kwa watumiaji ili kuwezesha watumiaji wengi kujitokeza kusajiliwa lakini pia kuweza kununua kemikali hizo kwa wafanyabishara wanaotambulika na kuzingatia matumizi salama ya kemikali hizo.

Copyright ©2022 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.