Mkemia Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Farid Mpatani, amesisitiza kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji na kiuchunguzi wa kimaabara na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Tanzania Bara.
Dkt. Mpatani, amesema hayo Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi aliyofanya katika ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali Tanzania Bara yenye lengo la kujifunza na kuimarisha uhusiano wa kikazi kati ya taasisi hizi mbili za kisayansi.
“Lengo la kwanza la kuja hapa ni kwa ajili ya kujifunza katika masuala mbalimbali ya kiutendaji na kimaabara na lengo la pili ni kuimarisha undugu wetu ambao umeanza zamani mahusiano mazuri baina ya taasisi hizi mbili, kwa kweli ziara hii tumejifunza mambo mengi sana, hasa kwenye masuala ya utendaji kazi tofauti, masuala ya uchunguzi wa kimaabara ambapo tuweza kutembelea saba tofauti kama ya chakula na dawa, maabara za sayansi jinai Vinasaba, Kemia na Toksikolojia, Maikrobaiolojia na mazingira ambazo zimetupa upeo mkubwa wa namna wa kuondoka na taaluma nzuri ya kwenda kufanyia kazi kule Zanzibar,” alisema.
Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar amesema taaluma na ujuzi ambao wameupata kupitia ziara hiyo wameuchukua na wataenda kuufanyia kazi ili kuweza kuimarisha utendaji kazi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar na kuimarisha uhusiano wa taasisi hizi mbili.
“Lengo letu ni kuchukua ujuzi huu ili kuimarisha utendaji kazi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar, tumefurahia ziara hii ya kikazi na tunaahidi ushirikiano wetu utaendelea kuimarika Zaidi ili kuboresha utendaji kazi wetu” alimaliza.
Naye Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, akiongea kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bara, amesema ziara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar imeendelea kuimarisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar.
“Kupitia ziara hii naamini Watendaji Wakuu na watumishi wengine tunakuwa pamoja katika kuhakikisha maabara za taasisi hizi mbili zinafanyakazi pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana utaalam na wataalam ili maabara zetu ziweze kufanya vizuri na kuwahudumia wananchi na Serikali zetu kadri zinavyotarajiwa” alimaliza.