CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe amewataka wanafunzi wa sekondari katika Wilaya ya Handeni kupenda kusoma masomo ya sayansi kwa sababu dunia ya sasa inaendeshwa na mapinduzi ya sayansi na teknolojia.

Siriel Mchembe ameyasema hayo jana wakati akipokea mchango wa vitabu 786 vya sayansi ya kidato cha tano na sita na kemikali kwa ajili ya maabara za shule kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mkata wilayani Handeni.

“Kupitia Sera ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha watoto wengi nchini wanajifunza masomo ya sayansi, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewezesha kutupatia vifaa mbalimbali vya shule vikiwemo kemikali za maabara kwa ajili ya masomo kwa vitendo na vitabu vya masomo ya sayansi nakala 786, ili kuhakikisha wanafunzi wetu wanajifunza na kupenda masomo ya sayansi ili kuendana na maendeleo ya sasa ya dunia ambayo inaendeshwa kwa mabadiliko ya kila siku ya sayansi na teknolojia.

“kutokana na kasi ya dunia katika maendeleo ya kisayansi walimu, wazazi pamoja na jamii kwa ujumla tunatakiwa kuwahamasisha watoto wetu kusoma masomo ya sayansi ikiwemo biolojia, fizikia, kemia na hisabati kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu katika masomo ya Sayansi na kutengeneza kizazi cha wataalam wengi wa sayansi kwa nchi kwa sababu kupitia sayansi tutatengeneza madaktari, wahandisi, walimu na wakemia na wajiolojia wengi katika nchi,” amesema Mchembe.

Aidha, Mkuu wa wilaya, ameipongeza Serikali kwa kuongeza idadi ya maabara na ujenzi wa madarasa zaidi ya 77 wilayani humo na pia kutatua changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi kwa kuongeza zaidi ya walimu 40 ambao wameongeza nguvu kubwa na kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kujifunza vizuri.

Naye, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, ametoa wito kwa wanafunzi kutumia vitabu na kemikali za maabara kwa ajili ya kujifunza kwa bidii na kuipenda sayansi, pia wafahamu kuwa sayansi na teknolojia ndiyo zinaleta maendeleo na kuwataka kutambua kuwa Serikali inawathamini kwa kuhakikisha inawajengea madarasa, kuwaletea walimu na vifaa vya kusomea.

“Tuna matumaini vitabu hivi vya sayansi na kemikali za maabara zitaweza kusaidia shule hii kujenga wataalam wa sayansi hasa ukizingatia serikali inaweka juhudi ili nchi yetu kufikia uchumi wa juu katika sayansi na teknolojia. Aidha, ni muhimu kuwekeza katika rasilimali watu na kujenga Watanzania wenye weledi. Nasi tutaendeleza lengo letu ambalo ni kuendelea kuwezesha vijana kufikia malengo yao kupitia elimu” alisema.

Aidha, Afisa Elimu Sekondari Handeni, John Lupenza, ameongeza kuwa Shule za Sekondari wilayani Handeni, zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu, maabara za kutosha pamoja na vitabu hali ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi kukimbia masomo ya Sayansi.

“Tunaishukuru sana Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa msaada huu wa vitabu na kemikali mbalimbali za maabara, matumaini yangu tutaweza kusonga mbele na vifaa hivi vitasadia hata wanafunzi kuweza kujisomea huku akiwaasa wanafunzi kutumia fursa hiyo kufaulu masomo ya sayansi,” alimaliza Lupenza.

 

Copyright ©2022 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.