CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na viongozi wengine wa Serikali wameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika utendaji kazi hasa katika masuala ya uchunguzi wa kimaabara na utoaji wa ripoti za uchunguzi kwa wakati.

Viongozi hao wamesema hayo wakati walipotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Januari 22-29, 2023.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mustapher Siyani, amepongeza maboresho ya makubwa yaliyofanywa na Mamlaka katika masuala ya kiuchunguzi wa kimaabara na kupelekea ripoti kutoka kwa wakati na kusaidia kusukuma mashauri ya kesi mbalimbali katika Mahakama.

“nawapongeza kwa maboresho ya kiutendaji mliyofanya ambayo yamesaidia kupunguza siku za uchunguzi na ripoti kutoka kwa wakati na kusaidia mashauri kwenda kwa haraka mahakamani. Nashauri Mamlaka kuongeza ubunifu zaidi katika utendaji kazi ikiwemo kubuni mbinu au mnyororo ambao utawezesha kupunguza siku za uchunguzi ukilinganishi na hizi za sasa hivi” alisema.  

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel, amepongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuanzisha mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Uchunguzi wa Maabara ambao utajumuisha wadau wa Jukwaa la Haki Jinai kuweza kubadilishana taarifa na kujua mnyororo wa uchunguzi wa sampuli mbalimbali zilizowasilishwa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

“Nawapongeza kwa kuanzisha mfumo wa TEHAMA wa Usimamizi wa Taarifa za uchunguzi wa Maabara (LIMS) ambao utasaidia kubadilishana taarifa kati ya Mahakama na wadau wengine wa jukwaa la Haki Jinai. Kwa upande wetu Mahakama nimeshasaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hivyo, anatarajia upande wenu kukamilisha mchakato huo ili kuanza utekelezaji wake ili kuongeza ufanisi katika utoaji haki kwa wakati mahakamani” alisema.

Aidha, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Shabani Lila, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ufanisi mkubwa wa utendaji kazi kwa sasa kwa sababu ripoti za uchunguzi wa kimaabara zinatoka kwa wakati na kurahisisha uendeshaji wa kesi mbalimbali ambazo zinahitaji majibu ya ripoti za kimaabara kutoka Mamlaka.

Kwa upande wa Kamishna wa Huduma za Sheria wa Jeshi la Uhamiaji, Novaita Mrosso, aliishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano mzuri inaoutoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Uhamiaji pale wanapohitaji msaada wa haraka kwenye masuala ya uchunguzi wa kimaabara.

“Nawapongeza sana kwa utendaji wenu kwani mashauri mengi ya Uhamiaji ambayo yalihitaji uchunguzi wa kimaabara kujua uhalali wa uraia wa baadhi ya waombaji wa hati za kusafiria yalifanyiwa kazi kwa haraka na kuwezesha Jeshi la Uhamiaji kufanya maamuzi sahihi kulingana na ripoti hizo za uchunguzi. Naomba muendelea kutoa ushirikiano kila tutakapohitaji msaada wa kuwezesha kutambua uhalali wa uraia kwa baadhi ya wananchi ambao wanakuwa na utata na wanahitaji hati za kusafiria za Tanzania” alimalizia.

Copyright ©2023 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.