Wachimbaji wadogo wa madini wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya wamenufaika na Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Madini na fursa za uwekezaji kwa kupata elimu kutoka kwa taasisi mbalimbali za Serikali.
Akizungumza wakati akifunga maonesho hayo katika viwanja wa Sinjiriri wilayani Chunya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera, amesema kupitia maonesho hayo, wananchi wa Mkoa wa Mbeya haswa wachimbaji na wadau wa madini wamejifunza mambo mengi yanayolenga shughuli za madini kupitia taasisi zilizoshiriki katika maonesho hayo ambayo yaliyoanza Machi 14 hadi 18, 2023.
“Wachimbaji wamejifunza njia mbalimbali ambazo ni sahihi kwa uchimbaji na uchenjuaji wa madini na namna bora ya matumizi ya vitendea kazi ambapo wataendelea kuzalisha kwa tija na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Homera, aliongeza kwa kuzitaka taasisi za Serikali kuendelea kuwaunga mkono wachimbaji wadogo kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu pamoja na kuendelea kutoa elimu juu ya uchimbaji salama wa madini ili kuleta ufanisi katika kazi zao.
Naye, Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya (MBELEMA), Leonard Manyesha, ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini, kuyafanya maonesho hayo kufanyika kila mwaka ili wachimbaji waweze kukutana na taasisi za Serikali na wadau wa madini ili kusaidia kutatua changamoto zao na kuwapa mbinu mbalimbali za uchimbaji, lakini pia alieleza kutatua changamoto ambazo wachimbaji wanazipitia.
Aidha, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya, ilishiriki maonesho hayo ikiwa ni taasisi ambayo inasimamia Sheria ya Kemikali za majumbani na viwandani, namba 3 ya mwaka 2003.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jansen Bilaro, amesema kuwa pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu, Mamlaka pia imeweza kusajili baadhi ya wadau.
“Kutoa elimu kwa wadau na wananchi katika maonesho haya ni moja la jukumu la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo tunaelezea namna mbalimbali ya matumizi ya kemikali, tabia zake na namna ya kujikinga ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea endapo usalama haujazingatiwa,” alisema Jansen.