Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias, amewataka Wajumbe wapya wa Baraza la Saba la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuzingatia mafunzo na kutambua jukumu la jumbe wa Baraza la Wafanyakazi kwa lengo la kuboresha utendaji wa Baraza na kuwa majadiliano chanya yenye kujenga na kuwezesha Mamlaka kufikia malengo.
Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali amesema hayo leo wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wapya wa Baraza la Saba yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Jengo la PSSSF, Dar es Salaam.
“Kwa kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali amewekeza rasilimali muda na fedha katika mafunzo haya, tunatarajia wajumbe kupata uelewa zaidi juu ya majukumu ya mjumbe wa Baraza na namna ya kuboresha zaidi majadiliano yetu ili kutoa ushauri chanya ambao utawezesha Mamlaka kufikia malengo yake, mazingira ya kufanyia kazi kuboreshwa zaidi, jamii ya Tanzania kupata huduma bora zaidi na Nchi yetu kufaidika zaidi kwa uwapo wa Taasisi hii.
Katika historia ya Mabaraza ya Wafanyakazi wa Mamlaka, Baraza hili ni Baraza la Saba ambalo linafanya kikao chake cha Kwanza. Majadiliano ambayo yamekuwa yakifanyika katika vikao vya Baraza yaliyopita yamekuwa shirikishi kwa kiwango cha juu na kuwezesha kutoka na maazimio ambayo yameiwezesha Menejimenti kufanya kazi nzuri ya kuisogeza Taasisi yetu mbele zaidi na kuboresha huduma zitolewazo na Mamlaka’’ alisema.
Mjumbe wa Baraza, Emanuel Lewanga, akiongea wakati wa mafunzo hayo aliwasihi wajumbe kuzingatia maelekezo ya Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuwezesha kuwa na Baraza lenye tija na litakalowezesha kuboresha maslahi ya Watumishi na utoaji huduma bora kwa wananchi. Vile vile, alisifu wawezeshaji wa mafunzo kwa kuwasilisha mada ambazo zimewapa uelewa wa kutosha juu ya majukumu, wajibu na haki za wajumbe wa Baraza na Menejimenti kwa ujumla.