CHIEF GOVERNMENT CHEMIST

Welcome to the Government Chemist Laboratory Authority (GCLA),your number one centre for laboratory analysis of samples/exhibits related to Forensic Sciences in order to facilitate forensic investigations and hence assurance of justice and rule of law,Read More>>

Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kaskazini, Arusha wametakiwa kumpa ushirikiano wa kikazi Meneja Eliamini Mkenga aliyehamishiwa Kanda hiyo.Hayo yamesemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, wakati akimtambulisha Meneja huyo baada ya kuripoti katika ofisi ya Kanda ya Kaskazini iliyopo jijini Arusha.

“Meneja ni mtu wa kazi  na anajua majukumu ya Mamlaka vizuri.  Ili kwenda pamoja naye mnatakiwa kufanya kazi kwa bidii maana yeye ni mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno.  Mnatakiwa kumpa ushirikiano wa kutosha maana hawezi kufanikisha bila ninyi, wote tunapaswa kufanya kazi ili kuboresha utendaji wa kanda hii maana ni moja ya Kanda muhimu kwa utekelezaji wa majukumu yetu. Meneja Mkenga ni mzoefu kwenye uongozi na anajua tafsiri za sheria, kanuni, taratibu za Utumishi wa Umma pamoja na miongozo mbalimbali ya Mamlaka, na kila anachotekeleza ni kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hivyo, watumishi pia tunapaswa kuzingatia hayo katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku” alisema.

Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amewataka watumishi kuwa na umoja na kuheshimiana kulingana na madaraja ya kiuongozi. Lengo likiwa ni kutimiza majukumu ya kazi na kuwa na utaratibu wa kukaa vikao vya pamoja na kuelezana ukweli kwenye vikao na kwa lugha nzuri.   

“Muwe na umoja lakini pia mheshimu ngazi za uongozi kuanzia meneja mpaka wasimamizi wengine ambao mmewachagua au wameteuliwa kuwaongoza, muendeleze ushirikiano kati yenu na kufanya kazi kwa ufanisi na kuepuka mrundikano wa kazi na mafaili kwa sababu hiyo haileti muonekano mzuri kwa wadau wa Mamlaka.  Tunapaswa kuongeza ubunifu kwenye utendaji wa kazi ili kuongeza tija na mapato ya kanda ambayo yatasaidia pia kuboresha maslahi ya watumishi” alimaliza.

Naye Meneja mpya wa Kanda, Eliamini Mkenga, akiongea amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kumteua na kuona anastahili kuongoza Kanda hiyo baada ya kustaafu kwa Meneja aliyekuwepo, Bw. Christopher Anyango. Amewaomba watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kulingana na majukumu waliyopangiwa.

“Nakushukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuongoza watumishi wenzangu katika Kanda hii, ninachowasihi watumishi wa Ofisi ya Kanda ni tujitume na kufanyakazi kwa weledi na bidii na kila aliyepewa jukumu atekeleze na akija kwangu awe amefanya maamuzi au kuleta mapendekezo yanayosaidia kufanya maamuzi. Kanda ina vijana wenye nguvu ya kufanya kazi, hivyo, kila mmoja nitahitaji kujua eneo lake la kazi ili kuweza kumpima kulingana na utendaji wake” alimaliza.

Copyright ©2023 Government Chemist Laboratory Authority. All Rights Reserved.

Designed and Mantained by GCLA ICT Team.