Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

KAMATI YA KITAALAM YA KUDHIBITI MATUKIO YA SUMU YAAHIDI KUIMARISHA UTENDAJI

Imewekwa: 22 May, 2023
KAMATI YA KITAALAM YA KUDHIBITI MATUKIO YA SUMU YAAHIDI KUIMARISHA UTENDAJI

Kamati mpya ya Kitaalam ya Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, imeahidi kuendelea kudhibiti matukio ya sumu nchini kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya sumu na namna ya kukabiliana na matukio ya sumu.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati baada ya kuzinduliwa na Mkemia mkuu wa Serikali katika ukumbi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Aprili 5, 2023, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalam ya Kudhibiti Matukio ya Sumu, Profesa Amos Mwakigonja, amewataka wajumbe kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza ubunifu wa namna ya kukabiliana na changamoto za sumu nchini.

“Kamati hii ni Kamati ya Kitaalam ambayo imeundwa na wataalam kutoka kwenye taasisi na vitengo mbalimbali Serikalini, wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na Mamlaka kwani muamko ni mkubwa na shauku ya kutekeleza majukumu tuliyopangiwa,” alisema.

Profesa Mwakigonja alieleza kuwa, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Kamati itashauri kuongeza tija na juhudi za kutangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili elimu juu ya sumu iweze kuenea kwa wananchi lengo likiwa kupunguza ajali zitokanazo na matukio ya sumu nchini.

Aidha, Mwenyekiti ameishauri Mamlaka kuendelea kufanya tafiti mbalimbali kwenye sumu na kuboresha mawasiliano kati ya Mamlaka na Taasisi nyingine za Serikali ambazo shughuli zake zinaingiliana na za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kama Maabara ya Afya ya Jamii, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), ambazo zikishirikiana zitaweza kuboresha ufanisi na kuleta matokeo chanya katika jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Yohana Goshashy, alieleza kuwa jukumu kubwa la Kamati ya Kitaalam ya Kudhibiti Matukio ya Sumu, ni kumshauri Mkemia Mkuu wa Serikali, katika shughuli zote za uendeshaji wa Kituo hicho na ameahidi kutoa ushirikiano kwa Kamati ili kwa pamoja waweze kufikia malengo ya kituo hicho.

Kamati hiyo inaundwa na wajumbe sita kutoka Wizara ya Afya, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Jeshi la Polisi.