Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAADHIMISHO YA MEI MOSI 2023

Imewekwa: 22 May, 2023
MAADHIMISHO YA MEI MOSI 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali inatambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa huku akiwasihi wafanyakazi kufanya kazi yenye weledi, moyo kwa kujituma ili taifa liweze kuendelea na kujenga uchumi imara.

Rais Samia, ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro.

“Siku ya leo (Mei Mosi), ni siku ya kutambua na kufurahia mchango wetu wafanyakazi kwenye uchumi na ustawi wa taifa letu. Ni siku ya kuonesha heshima na kutoa shukrani kwa wafanyakazi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa taifa,” alisema Dkt. Samia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Evaclotida Kapinga, amewashukuru watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kwa ushirikiano waliouonesha katika mwaka mzima toka maadhimisho ya Mei Mosi ya mwaka jana hadi mwaka huu, kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi na kama alivyoelekeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa kujituma.

“Kupitia agizo la Mheshimiwa Rais, wafanyakazi tutachangia kwenye maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, kwani uchumi wetu ukikua maslahi pia yataboreshwa,” alisisitiza Mkurugenzi.

Naye, Leonidas Daniel, ambaye alichaguliwa kuwa Mtumishi Hodari kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, amewasihi watumishi wa Mamlaka kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao na viongozi na pia kutumia taaluma zao kuleta ubunifu kwenye majukumu yao pamoja na kufanya kazi kuendana na ukuaji wa teknolojia.