Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

RAIS SAMIA ATAKA KASI KUONGEZEKA UPIGAJI VITA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Imewekwa: 27 Jun, 2023
RAIS SAMIA ATAKA KASI KUONGEZEKA UPIGAJI VITA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Asasi za Kiraia pamoja na wazazi na walezi kuwekeza nguvu zaidi katika kulinda jamii kwa kuendelea kudhibiti uingizaji, uzalishaji, usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya.

Mhe. Rais, aliyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani iliyobeba kaulimbiu ‘Zingatia Utu, Imarisha Huduma za Kinga na Tiba iliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Juni 25, 2023.

“Kinga ni bora kuliko tiba, hivyo natoa wito kwa Mamlaka husika, Taasisi za Serikali na Asasi za Kiraia, kuongeza jitihada kwenye kutoa elimu kwa jamii hasa kwa vijana ili wajiepushe na matumizi ya dawa za kulevya, lakini na sisi Serikali tumejipanga vyema kukabiliana na janga hili,” Alisisitiza Mheshimiwa Rais.

Pia, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa rai kwa Mamlaka na Taasisi zinazohusika na masuala ya dawa za kulevya kufanya kazi kwa weledi kwa kuhakikisha watuhumiwa wa dawa za kulevya wanapata haki zao kwa wakati bila kuchelewesha kesi mahakamani.

Aidha, Rais Samia, aliipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kwa kufanya kazi vizuri katika udhibiti wa uingizaji wa kemikali bashirifu nchini na pia kuendelea kushirikiana na Mamlaka zinazohusika na upigaji vita dawa za kulevya nchini.

Katika Maadhimisho hayo ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyoanza Juni 23 hadi 25, 2023, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), ilitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Mamlaka kuhusu shughuli mbalimbali wanazozifanya, lakini pia kupitia wataalam kutoka GCLA, waliweza kupima na kutambua utumiaji wa aina mbalimbali ya dawa za kulevya kutoka kwa wahanga, kama vile heroin, bhangi, mirungi na pia kutambua wale ambao tayari wapo kwenye tiba ambao wanatumia dawa ya methadone.