WAJASIRIAMALI WAASWA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI
Wajasiriamali wadogo na kati Wanaozalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na Kemikali mkoani Tanga, wametakiwa kutumia kemikali hizo kwa usalama ili zisiweze kuleta madhara pindi wanapokuwa wakizitumia, kwani endapo zitatumika bila kuzingatia usalama, zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na kuleta athari katika mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Joseph Kaji, amesema hayo wakati wa akifungua mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kwa Wajasiriamali hao yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, kwa kushirikiana na SIDO Mkoa wa Tanga.
"Kemikali ni nzuri ukiitumia vizuri ila ukiitumia vibaya ina madhara makubwa.
Kemikali mkiitumia vizuri itawanyanyua ila mkifanya mchezo ni hatari, nawaomba ,msikilize kwa makini mafunzo haya na mkitoka hapa mkawe mabalozi wazuri kwa wajasiriamali wenzenu ambao wanatumia kemikali, wafikishieni elimu hii mtakayopatiwa, alisema Kaji.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kaskazini,Eliamini Mkenga, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha Wajasiriamali wadogo na wa kati namna sahihi ya matumizi salama ya kemikali, kuzalisha salama na kuhakikisha kila anayezungukwa na wazalishaji hao anakuwa salama dhidi ya madhara yanayoweza kuletwa na kemikali.
" Kila mtu ana haki ya kujua aina ya kemikali anayoitumia, kwa kujua madhara yake, namna ya kujikinga lakini pia atahadhalishe jamii yake namna ya kujikinga na kutumia kwa kuzingatia usalama. Hivyo mafunzo hayo ni muhimu kwa Wajasiriamali hawa na lazima tufahamu kemikali ni rafiki lakini kuna muda si rafiki na unatakiwa kuwa nayo makini" alisema Mkenga
Aidha, Mtenga amesema mafunzo hayo ambayo yanatolewa na Mamlaka hiyo ni muhimu kwa Wajasiriamali wanaotumia kemikali na sio kuyadharau, kwani yakitumika vizuri yatasaidia wajasiriamali hao kuweza kusonga mbele zaidi na hata kufikia kuwa wazalishaji wakubwa na si wadogo au kati.
Naye Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Tanga, Niko Mahinya, amesema mafunzo hayo si muhimu tu kwa wazalishaji hao, bali yanasaidia kuwakinga hata watumiaji wa bidhaa zitakazolishwa na wajasiriamali hao, kwani wataweza kuzalisha bidhaa ambazo zitakuwa salama na ambazo haziwezi kuwadhuru watumiaji wa bidhaa hizo.
Zaidi ya Wajasiriliamali wadogo na kati zaidi 150 kutoka Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Tanga, wameweza kushiriki kwenye mafunzo hayo ya siku mbili ya matumizi salama ya kemikali ambayo yameandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na SIDO.