Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WASIMAMIZI WA KEMIKALI WATAKIWA KUZINGATIA USALAMA

Imewekwa: 09 Oct, 2023
WASIMAMIZI WA KEMIKALI WATAKIWA KUZINGATIA USALAMA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki, imetoa mafunzo kwa wasimamizi wa kemikali kwa lengo la kuhakikisha wanawasimamia vyema wasafirishaji, wapakiaji na watunzaji wa kemikali ili kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo salama ya kemikali pamoja na kuzingatia usalama wa nchi.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Sabanitho Mtega aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa kemikali kutoka kampuni mbalimbali zinazojihusisha na kemikali yaliyofanyika katika ukumbi wa Mamlaka jijini Dar es Salaam, Septemba 20, 2023.

"Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo Wasimamizi wa Kemikali katika kujua madhara ya kemikali, faida za kemikali lakini pia wawe kwenye nafasi chanya ya kuwaelimisha wafanyakazi waliopo chini yao kwenye maeneo yao ya kazi. Elimu hii iwe chachu kwa wasimamizi wa kemikali kwa kufanya kazi kwa weledi katika suala zima la kemikali, hivyo kuimarisha jitihada za utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya mwaka 2003 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2020," alisema Mtega.

Pia, Mtega amewataka wasimamizi hao wa kemikali kuwa mabalozi wa kuhamasisha wadau wengi zaidi kupata mafunzo hayo pamoja na kueneza elimu ya matumizi salama ya kemikali katika maeneo yao ya kazi ili kulinda afya za binadamu, wanyama na mazingira.

Naye, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, ametoa rai kwa wasimamizi wa kemikali kuhakikisha wanatenga bajeti ya kununua vifaa kinga kwa ajili ya makundi mbalimbali yanayojishughulisha na kemikali wakiwemo madereva, wapakiaji na wasambazaji.

Kwa upande wake Mwanasheria wa kampuni ya Morogoro Plastics, Winfrida Gavana amesema kuwa mafunzo hayo waliyopewa yana manufaa makubwa kwao kama  wasimamizi wa kemikali, hivyo kwa kuzingatia Sheria za kemikali watahakikisha wanazingatia matumizi salama na sahihi ya kemikali katika uzalishaji.