Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATUMISHI WA MAMLAKA WATAKIWA KUIMARISHA MISINGI YA UTOAJI HUDUMA

Imewekwa: 15 Nov, 2023
WATUMISHI WA MAMLAKA WATAKIWA KUIMARISHA MISINGI YA UTOAJI HUDUMA

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko  amewataka watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wanaowahudumia.

Akizungumza wakati akifungua Mafunzo ya siku moja ya Huduma kwa Mteja yaliyofanyika katika ukumbi wa Mamlaka jijini Dodoma Novemba 10, 2023. Mkemia Mkuu wa Serikali alisema kuwa Mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanasaidia kuimarisha utoaji huduma kwa wateja.

“Tutambue jukumu letu la msingi na kila mmoja kwenye taasisi aelewe kwamba ana wajibu wakufahamu majukumu ya Mamlaka, huduma na maeneo anayofanyia kazi ili mteja anapokuja awe na uwezo wa kumuelekeza, kumuhudumia lakini na kutambua kwamba tunahitaji kutokuwa na urasimu, kutoa huduma zilizo bora na uwajibikaji wa pamoja,” alisema Dkt. Mafumiko.

 Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa, kutoa huduma bora kutaongeza ubunifu lakini pia kubadilika kimtazamo kwasababu Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali haisimami yenyewe bali ni taasisi mtambuka hivyo ni vyema kuongeza tija zaidi.

Naye, mwezeshaji wa mafunzo ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Sylvester Omary alisema utoaji wa huduma bora kwa mteja ni njia mojawapo ya kujitangaza hivyo ni muhimu kwa kila mtumishi kufanya jitihada za kubadili mtazamo na kuwa na mtazamo chanya ili kuweza kuwahudumia wateja kwa namna bora zaidi. Pia, amewaasa watumishi kufanya kazi kwa mshikamano na upendo ili kuweza kujenga mahusiano mazuri baina ya watumishi wenyewe na watumishi kwa wateja.

Kwa upande wake Mkemia Zabibu Duru, ameahidi kuzingatia mafunzo hayo kwa kuendelea kuwakilisha vyema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika utoaji huduma bora kwa mteja na kuhakikisha mteja anaridhika na huduma za Mamlaka.

“Tumefarijika baada ya kupata elimu hii ya huduma kwa mteja maana imetujenga na kwa muktadha huo, ili kujenga na kulinda jina la taasisi tunapaswa kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wetu,” alisema Zabibu.