Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefanikiwa kuibuka mshindi ya pili katika Maonesho ya Arobaini na tatu (43) ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Saba saba kwenye kipengele cha Mamlaka za Usimamizi na Udhibiti zinazotoa huduma bora katika maonesho hayo yaliyoanza Juni 28 mpaka 13 Julai 2019, kwenye Viwanja vya Saba saba vilivyopo barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Mamlaka imefanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kukidhi vigezo vilivyokuwa vimewekwa na majaji wa zoezi hilo. Baadhi ya vigezo hivyo vikiwa ni usimamizi bora wa majukumu kama Mamlaka ya udhibiti na utoaji huduma bora na za kuridhisha kwa wateja wanaotembelea banda husika ikiwemo ufafanuzi wa shughuli zinazofanywa na Taasisi, uwezo wa watumishi kuelezea majukumu ya taasisi kwa wateja na wadau wanaotembelea banda, uwepo wa huduma halisi zinazotolewa na taasisi, maandalizi ya banda na maonesho ya kazi za Mamlaka na kuweza kuoanisha kwa vitendo kauli mbiu ya maonesho na huduma za Taasisi.
Akiongea baada ya kupokea zawadi ya ushindi kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, aliwapongeza washiriki na watumishi wote wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kujituma, ushirikiano na weledi katika kufanikisha ushindi huo.
“Napenda kuwapongeza kwa ushindi huu maana ni ushindi wa Taasisi nzima kutokana na kuwepo kwa mchango wa kila mmoja katika kufanikisha ushindi huu kwa mara ya pili mfululizo tunashika nafasi ya pili. Ni fahari kwetu na faraja kwa kuendelea kushinda na hii inaonyesha kwamba elimu tunayotoa kwa umma inasaidia jamii kufahamu majukumu yetu, hivyo ni jambo la kujivunia. Tunachopaswa kufanya kwa sasa ni kujipanga zaidi ili mwakani kushinda nafasi ya kwanza kwa kuboresha zaidi ushiriki wetu na kuangalia pale ambapo kumetupunguzia nafasi ya kushika nafasi ya kwanza kwa mwaka huu.
Naamini huu ni mwanzo tu wa kuendelea kutoa elimu na huduma nzuri zaidi kupitia Mamlaka na kuwafikia zaidi wateja na wadau wetu kwa lengo la kuwafanya wafahamu zaidi shughuli na huduma zote zitolewazo na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.”
Katika kipengele hicho taasisi iliyoshika nafasi ya kwanza ilikuwa ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na nafasi ya tatu ikishikwa na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).