Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri, ameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki kwa kuandaa mafunzo kwa Maafisa Biashara wa Wilaya ya Ilala kwa sababu mafunzo waliyopata yatawasaidia katika kuwatambua wafanyabiashara wanaojihusisha na kemikali wanapokuja kuomba leseni za biashara.
Akiongea leo wakati wa kufunga mafunzo kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani inayosimamiwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali , Mkurugenzi Jumanne Shauri, amesema anaamini mafunzo hayo yataongeza ufanisi na weledi kwa Maafisa Biashara katika kuwatambua wafanyabiashara wa kemikali watakapofika kuhitaji leseni hivyo kuwaelekeza kwanza kusajiliwa na Mamlaka.
“Nimefarijika sana kwa mafunzo kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali naamini yatawaongezea weledi kwa Maafisa Biashara katika majukumu yao ya utoaji leseni kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara za kemikali. Itasaidia kutoruhusu watu wafanye biashara ya kemikali bila kuwa na vibali na kusajiliwa na Mamlaka. Tutahakikisha Maafisa Biashara wa Manispaa ya Ilala tunashirikiana na Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki katika kuhakikisha wanapata barua za utambulisho au usajili kabla ya kupewa leseni ya biashara.”
Mkurugenzi aliendelea kwa kusema kwamba watashiriki katika kufanya ukaguzi wa kutambua wafanyabiashara ambao walipewa leseni za biashara na wanajihusisha na biashara ya kemikali bila kutambuliwa na Mamlaka kwa lengo la kusaidia wasajiliwe ili kulinda pia afya za wananchi na mazingira kwa sababu kemikali ni hatari zisiposimamiwa kikamilifu.
“Itabidi kufanya ukaguzi wa maduka yanayouza kemikali ili kuweza kutambua kama wamesajili lengo ni kuwalinda walaji. Tutashirikiana kutambua kemikali zinazouzwa hazina madhara kwa watumiaji na wahusika wamesajiliwa ili kulinda afya zetu na mazingira” alimaliza. Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Biashara 39 kutoka Manispaa ya Ilala.