Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Mabula Mchembe ametoa wito kwa Taasisi na Wataalam wa Kemia na Fizikia nchini, kutumia taaluma hizo kushiriki katika utatuzi wa majanga mbalimbali pindi yanapojitokeza nchini.
Profesa Mchembe, Prof Mchembe ametoa wito huo Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya Kuwapongeza na kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya Kemia, Fizikia na Bailojia katika mitihani ya kidato cha nne na sita kwa mwaka 2018/2019 kama sehemu ya kutoa motisha na hamasa kwa wanafunzi kuweza kusoma masomo ya Sayansi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam.
“Natoa wito kwa Taasisi na Wataalam wa Kemia na Fizikia nchini, kutumia taaluma hizo kushiriki katika utatuzi wa majanga mbalimbali pindi yanapojitokeza nchini kama inavyofanya Mamlaka ya Maabara ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) hatua ambayo itasaidia kudhibiti au kuondoa madhara makubwa ambayo yalikuwa yasababishwe kupitia majanga hayo.
Haitawezekana bila mchango wa Wataalam waliosoma masomo ya Kemia, Fizikia na Baiolojia, hivyo tuwaombe kuweza kusaidia kufanikisha utatuzi wa matatizo mengi yanayotokea na kuhitaji Wataalam katika taaluma hizo.”
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema Mamlaka imeendelea kutoa zawadi hizo kama kuongeza hamasa kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.
“Mamlaka imekuwa ikiendelea na utaratibu huu wa kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi wa kike na wa kiume wa kidato cha nne na kidato cha sita pamoja na walimu wao kwa kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya Taifa kwa masomo ya Kemia na Baiolojia kila mwaka kwa lengo lile lile la kuleta chachu kwa vijana wetu kupenda zaidi masomo ya sayansi.
Aidha, napenda nitumie nafasi hii kukujulisha wewe mgeni rasimu na wageni waalikwa kuwa, mwaka huu tumeendelea kupanua zaidi utoaji wa zawadi hizi kwa kuongeza somo la Fizikia kuwa mojawapo ya somo ambalo wanafunzi wa kike na wa kiume pamoja na walimu wao waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya Taifa ya kidato cha nne na kidato cha sita kupongezwa na kupewa zawadi.“