Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA YAPOKEA TUZO YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Imewekwa: 22 Jul, 2024
MAMLAKA YAPOKEA TUZO YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias, Leo 17 Julai, 2024 amepokea tuzo kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko ya kutambua mchango wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo.

Akikabidhi tuzo hizo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kamishna Jenerali amesema tuzo hizo ni katika kutambua na kuheshimu mchango mkubwa wa wadau mbalimbali na Mamlaka zingine za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika Mapambano dhidi ya Dawa za kulevya nchini.

Tunatambua mchango wao mkubwa, vita dhidi ya dawa za kulevya si jambo rahisi inahitaji ujasiri, kujitolea na moyo wa dhati katika kupambana na tatizo hili kubwa linalo ikabili taifa letu na dunia kwa ujumla, kupitia kazi zao wadau hawa wameweza kuokoa maisha, kutoa matumaini na kusaidia kujenga mustakabali bora kwa vijana wetu na kizazi kijacho na sisi  tunawapa tuzo na vyeti kama ishara ya shukrani na kuthamini mchango wao mzuri kwa Mamlaka ya  Dawa za kulevya” amesema.

Hata hivyo ametoa onyo kwa wale wanaojishughulisha na kufadhili biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja na badala yake kujihusisha na biashara halali kwani uchunguzi dhidi yao unaendelea.

Akizungumza kuhusu dhamira ya serikali ya katika kupambana na dawa za kulevya nchini amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita  ni kujenga uchumi endelevu na ili kufikia malengo hayo ni lazima kuwalinda vijana ambao ndio nguvu kazi na wazalishaji wakuu.

“Kama Serikali tutahakikisha dawa za kulevya zinaisha nchini ambazo ndizo zinaua nguvu kazi za vijana wetu na kuharibu mnyororo mzima wa uchumi wetu”.  amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, amesema moja ya sababu za magonjwa kuongezeka mbali na teknolojia ya afya kupanda na Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali  ni utumiaji wa dawa za kulevya, kwa sababu matumizi ya dawa za kulevya hupelekea  watumiaji kupatwa na magonjwa mbalimbali  kama vile magonjwa ya afya ya akili, Saratani na homa ya Ini.

Akizungumza kwa niaba ya wadau waliopewa tuzo, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhaville, amesema wote waliopokea tuzo wanaamini kuwajibika katika kutoa mchango ili kusaidia kuwa na taifa lenye vijana wenye nguvu na busara kwa sababu wao ndio watakaoendeleza nchi.