Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WAAJIRIWA WAPYA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Imewekwa: 11 Jul, 2024
WAAJIRIWA WAPYA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Mkemia Mkuu wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt.Fidelice Mafumiko, amewataka waajiriwa wapya wa Mamlaka kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na miongozo ya utumishi wa umma na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwaingiza kwenye matukio ya rushwa.

Dkt. Mafumiko ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Mamlaka, ambapo amesema mafunzo hayo yatawasaidia kujua mifumo mbalimbali ya kiutumishi na utekelezaji wa majukumu mbalimbali ambayo Mamlaka imekabidhiwa na Serikali kuyatekeleza.

“Mimi Matarajio yangu kwenu ni makubwa sana, mnisaidie kutekeleza na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usimamizi wa kemikali, Serikali imetukabidhi jukumu hilo na lazima tulitekeleza kama sheria iliyoanzisha Mamlaka inavyotaka, alisema Dkt. Mafumiko.”

Aidha, Dkt. Mafumiko, amewataka waajiriwa hao kutokuwa sehemu ya walalamikaji kwa changamoto zilizopo ndani ya Mamlaka bali wawe sehemu ya suluhisho ya changamoto hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, aliwataka waajiriwa hao kuzingatia mafunzo wanayopatiwa kwani yatakuja kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya Mamlaka.

Kwa mujibu wa waraka namba 5 wa mwaka 2011 wa Utumishi, unaelekeza kila waajiriwa wapya ni lazima wapatiwe mafunzo elekezi ili kuwawezesha kufahamu uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi husika, pamoja na kufahamu sheria mbalimbali za utumishi na utawala bora.