WADAU WA KEMIKALI WAPEWA MBINU ZA USALAMA WA KEMIKALI
Wadau wanaojishughulisha na matumizi ya kemikali Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wamehimizwa kuzingatia Sheria na Kanuni za matumizi ya kemikali ili kuondokana na athari ambazo hujitokeza endapo kemikali hazitotumika kwa kuzingatia usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga alitoa wito huo wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi salama wa Kemikali kwa wadau wanaojihusisha na shughuli za kemikali katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika kuanzia Novemba 7 hadi 8, 2024 katika Hoteli ya Omary City iliyopo wilayani Chunya.
“Kemikali hutumika katika uchimbaji na uchakataji wa madini, hivyo kemikali hizi zinahitaji uangalifu katika kutumia, kutunza ili kuepuka kusababisha madhara mbalimbali kwa watumiaji, wauzaji, wanyama na mazingira,” alisema Mhe. Batenga.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ya usimamizi salama wa kemikali kwani uchimbaji wa madini huchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo Mamlaka iendelee kutoa elimu ya kemikali kwani wadau wapo wengi.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima amewataka wadau walioshiriki mafunzo ya usimamizi salama wa kemikali kuwa mabalozi kwa jamii lakini pia ametoa wito kwa wadau ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo, kuwa mafunzo hayo ni endelevu hivyo wawe tayari kushiriki wakati Mamlaka itakapotangaza tena.
“Hii elimu tutaendelea kutoa mara kwa mara kwa wadau na kuhakikisha kwamba kemikali zinatumika vizuri na hazileti madhara kwa watumiaji wenyewe, lakini pia na jamii inayowazunguka, alisema Mulima.
Naye Omary Hamisi kutoka kampuni ya Small Scale Miners - Chunya, ameishukuru Mamlaka kwa kuwafikia na kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa sababu wamekutana na mambo mengi ya kigeni kwenye masuala ya matumizi ya kemikali ikiwemo kuzifahamu sheria, alama za kemikali, utunzaji na namna ya utumiaji wa kemikali hatarishi.