WAKULIMA WASHAURIWA KUPIMA UDONGO
Kupima udongo kitaalam kabla ya kuanza shughuli za kilimo ina saidia kujua kiwango cha magadi yaliyopo katika ardhi kama yamezidi, yapo kawaida au yamepungua hivyo upimaji wa udongo utasaidia kufahamu maeneo ambayo hayana msaada kwa ajili ya kilimo.
Akizungumza katika Maonesho ya Nane nane Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima amewashauri wakulima kuwa na tabia ya kupima udongo kabla ya kulima ili kubaini afya ya udongo ili aweze kuutibu udongo kabla ya kuanza kulima. Mulima amesema hayo Agosti 4, 2024 katika viwanja vya nane nane vya John Mwakangale,jijini Mbeya.
“Mamlaka inafanya uchunguzi kubaini afya ya udongo maana udongo unaweza kuwa na tindi kali ambayo inaweza kuwa juu sana au iko chini. Hivyo, tunashauri wakulima kutembelea ofisi zetu ili kuweza kafanya vipimo kupitia wataalam waliobobea kwa kutumia mitambo ya kisasa kwa lengo la kuwasaidia wakulima waweze kunufaika na mazao,” alisema Mulima.
Aidha, Meneja alisema pia Mamlaka inachunguza vyakula vinavyozalishwa ili kujua ubora wake kama vile mahindi, karanga na mazao mbalimbali ili mkulima anapotafuta soko awe na uhakika wa ubora wa mazao yake. Ameongeza kuwa Mamlaka inachunguza asali ili kuangalia kama kuna mabaki ya viuatilifu kwa sababu ili asali iuzwe kimataifa lazima ichunguzwe ubora ili kubaini kama inaweza kufaa kwa matumizi ya binadamu.
Naye Msimamizi wa Dawati la Usajili, Georgina Kilindo, amawasihi wadau wa kemikali kutembelea banda la Mamlaka katika Maonesho ya Nane nane ili waweze kupata elimu kuhusu majukumu mbalimbali ya Mamlaka ikiwemo kufahamu taratibu za usajili wa wadau wanaojishughulisha na kemikali za viwandani na majumbani.
Kwa upande wake Salum Ulimwengu ambaye ni Afisa Masoko katika kampuni ya E – Fooding & Drinks, ameipongeza Mamlaka kwa jitihada za kuhakikisha inawafikia wadau wengi na kuwapatia elimu kuhusu majukumu inayotekeleza na pia amewashauri wadau mbalimbali kutembelea banda la Mamlaka na Ofisi zake ili waweze kupata maelezo na kujifunza zaidi.
“Nina furaha kubwa na nina shukuru sana kwa maswali ambayo tumeyauliza hapa na jinsi tulivyojibiwa, nikiri kwamba tumeridhika na tunaweza tukaendelea na miradi yetu katika siku zijazo haya yote kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema Ulimwengu.