WAPELELEZI WATAKIWA KUZINGATIA USHAHIDI WA KISAYANSI
Jeshi la Polisi mkoani Tabora limewataka maafisa upepelezi mkoani humo kutumia ushahidi wa kisayansi hasa katika makosa ya jinai ili waweze kutenda haki wanapokuwa mahakamani.
Rai hiyo imetolewa Julai 27,2024 na Mkuu wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,Twaha Lulengelule katika mafunzo ya namna bora ya uchukuaji wa sampuli za makosa ya jinai kwa maafisa upepelezi wa Jeshi la Polisi mkoani humo yaliyotolewa na wataalamu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Niishukuru Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mafunzo haya,ukizingatia sasa hivi Jeshi la Polisi tunajikita sana katika ushahidi wa kisayansi ushahidi ambao hauna mashaka wala hauna mgogoro wowote na Mkoa wa Tabora ni mkoa wenye matukio mengi ya mauaji, lakini pia makosa ya ubakaji na ulawiti yanakuja kwa wingi.
Hivyo, kwa kutumia ushahidi wa kisayansi hasa katika mauaji ambayo tunakutana na zana mbalimbali za mauaji, elimu hii itatuwezesha sasa kujua namna gani ya kuweza kupata sampuli na kuzihifadhi na kuzipeleka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na pia itatusaidia sana katika kuhakikisha haki inatendeka kwa maana ya kupeleka majalada vizuri na kuyafikisha Ofisi ya Mashitaka na kwenda mahakamani na kupata ushindi” alisema Lulengelule.
Kwa upande wake Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali, Fidelis Bugoye, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Jeshi la polisi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa umahili na weledi.
“Tumetumia fursa hii kuwambusha pia wenzetu wa Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao kwa umahili na weledi katika uchukuaji wa sampuli ili maabara za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ziweze kufanya uchunguzi kwa wakati na kutoa majibu yanayokusudiwa” alisema Bugoye.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata imewaongezea chachu ya kufanya kazi kwa umakini na weledi zaidi.
Takribani Askari 43 wa vitengo vya upelelezi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Tabora wameshiriki mafunzo hayo.