Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WASIMAMIZI WA KEMIKALI NCHINI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Imewekwa: 26 Jul, 2024
WASIMAMIZI WA KEMIKALI NCHINI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mohamed Mang’una amewataka Wasimamizi wa Kemikali nchini kufanyakazi kwa weledi kwa kufuata Sheria Kanuni na Taratibu za nchi kwa kuwa kazi wanayofanya imeshika usalama, uhai, na afya za watanzania wengi ikiwa ni  pamoja na wao wenyewe.

Mganga Mkuu ameyasema hayo Julai 24, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali maeneo ya kazi kwa Wasimamizi wa Kemikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila.

“Sisi kama watanzania tumedhamini maisha yetu mikononi mwenu ninyi mnaoshughulika na kemikali tunategemea kwamba kila mmoja wenu katika sekta yake na sehemu yake atafanyakazi kwa weledi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu, mkizingatia kuwa kazi mnayoifanya imebeba dhamana ya usalama wa afya na uhai wa watanzania wengi” Alisema.

Dkt. Mohamed amesema Kemikali ni kitu kizuri kwa kuwa inaleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa viwanda vingi vinatumia kemikali katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali lakini zisiposimamiwa vizuri zinaweza kuleta matatizo makubwa na udhibiti wake unaweza kuwa mgumu.

“Tanzania ni lango la nchi nyingi, kupitia bandari na njia zingine, nchi jirani na nchi zingine zinapitisha kemikali kupitia lango hilo, kwa hiyo mnapofanya kazi kwa weledi mnasaidia uchumi wa nchi kukua na pia kuongeza mashirikiano mazuri zaidi kwa sababu ya uhakika wa  kusafirisha bidhaa  zao kwa usalama” alimaliza.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, amesema lengo la mafunzo hayo kwa Wasimamizi wa kemikali ni kuongeza usimamizi na udhibiti wa kemikali, kwa sababu kundi hilo ndilo linalotoa maelekezo mbalimbali ya usimamizi wa kemikali kwa watumishi wao wanapokuwa kwenye  uzalishaji, utumiaji, usafirishaji au uchakataji wa kemikali taka.

Hata hivyo amesema kuwa elimu itakayotolewa itasaidia Mamlaka kupata taarifa mbalimbali za kemikali na hivyo kuongeza utekelezaji wa Usimamizi na Udhibiti wa Sheria ya Kemikali ambayo Mamlaka inaisimamia.

“Tunaamini elimu itakayotolewa hapa itasaidia kuongeza wigo wa kupata taarifa mbalimbali za kemikali, kwa sababu kemikali zitakuwa zikiingia kwa njia halali kwenye mipaka halali  na siyo njia za panya, hatutasikia matukio mbalimbali kama ya uchepushwaji wa kemikali zinazotumika kutengeneza vitu ambayo haviruhisiwi ikiwemo madawa ya kulevya”. Amesema.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Ernest Modest Mlenge, Meneja Uendeshaji kutoka kampuni ya Dar es Salaam Corrido group, amesema wamehudhuria mafunzo haya ili kupata elimu zaidi ya namna bora ya kuhifadhi kemikali ili zisiweze kuleta madhara kwa jamii na kwa mazingira na ameishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia wa Serikali kwa kuwapatia elimu ambayo itawapatia manufaa makubwa kwa vile watakuwa na uwezo mkubwa wa kushughulika na kemikali kwa ufasaha.