Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

JAMII YAHIMIZWA KUWAHAMASISHA WANAFUNZI KUSOMA MASOMO YA SAYANSI

02 Jun, 2023 - 30 Jun, 2023
20:00:00 - 17:00:00
JULIUS NYERERE CONVECTION CENTRE
Silvesta

Serikali imeendelea kuwaasa wazazi, walezi na jamii kuendelea kuhamasisha wanafunzi katika ngazi mbalimbali nchini kutambua umuhimu wa kusoma na kupenda masomo ya sayansi ili kuwatengeneza vijana kuwa wataalam wa kesho na kufikia malengo ya Mipango na Mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025).

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu, amesema hayo, Juni 1, 2023, katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi (Biolojia, Fizikia na Kemia), kwa kidato cha nne na sita kwa mwaka 2021 na 2022, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Sayansi inakua, na sisi kama wataalam ni lazima tuendelee kukua na kurithishana ujuzi na ufahamu unaoendelea kuboreshwa siku hadi siku. Ni lazima pia tufanye juhudi ya kuifanya jamii ione umuhimu wa sayansi na kutambua mchango kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla” alisema Profesa Nagu.

Aidha, Mganga Mkuu wa Serikali, alisema kuwa moja kati ya vipaumbele vya Wizara ya Afya ni Kulinda afya ya jamii na mazingira, ambapo amesema utekelezaji wa kipaumbele hiki utaweza kufanikiwa kwa kujenga misingi ya kuandaa vijana wanaomudu na kupenda masomo ya sayansi, sambamba na kuimarisha vyuo vya mafunzo kwa wataalam wa sekta ya afya ya jamii.

“Ninashukuru kwamba Mamlaka imebuni mbinu bora na mwafaka ya kuhamasisha vijana kupenda masomo ya sayansi. Ni imani yangu kuwa, kazi hii ya kuwatia moyo vijana wetu waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi itakuwa endelevu,” alisema.

Sambamba na hilo, Profesa Nagu, aliwapongeza Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu wa Serikali na watumishi wote wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kwa kazi nzuri, kubwa na ngumu ambayo wamekuwa wakiifanya kwa moyo wa dhati, uzalendo na uadilifu na kuwasihi kuendelea na juhudi na moyo huo huo ili kuhakikisha Mamlaka inaendelea kutoa huduma bora kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Naye, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya kazi kubwa na kuweka jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania, anapata elimu bora na stahiki katika ngazi zote ambapo miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuwapa hamasa na fursa watoto wa Kitanzania kupenda kusoma masomo ya sayansi, kuajiri walimu wa sayansi, kuondoa ada na kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya kujifunzia zikiwemo maabara.

Kwa upande wake mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi katika somo la Kemia Kidato cha Sita, Lucy Elias Magashi, alipongeza utoaji wa zawadi hizo na kutoa rai kwa Serikali kuendelea kuhamasisha wanafunzi waliopo mashuleni kuendelea kusoma kwa bidii masomo mbalimbali hasa ya sayansi pamoja na kuwawezesha ili waweze kutimiza ndoto zao.

JAMII YAHIMIZWA KUWAHAMASISHA WANAFUNZI KUSOMA MASOMO YA SAYANSI