Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YAPONGEZWA KWA KUTOA ELIMU KWA WADAU WA SAYANSI JINAI

Imewekwa: 11 Mar, 2025
GCLA YAPONGEZWA KWA KUTOA ELIMU KWA WADAU WA SAYANSI JINAI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt John Mboya, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa elimu ya uchukuaji, utunzaji na usafirishaji salama wa Sampuli za jinai kwa wadau waliopo katika mlolongo wa mashauri ya jinai kwa kuwa yatasaidia kutenda haki kwa jamii.

Dkt Mboya ameyasema hayo Machi 7, 2025 wakati akifungua mafunzo ya uchukuaji, utunzaji na usafirishaji wa sampuli za jinai kwa wadau wa sayansi jinai yaliyofanyika katika ukumbi wa JM Hotel mkoani Tabora.

“Nimshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuleta mafunzo haya muhimu  katika Mkoa wetu ambayo ninaamini yataleta tija kubwa katika mfumo mzima au mlolongo wa haki jinai katika jamii yetu, kwa kuhakikisha kwamba sampili zinazochukuliwa na kutunzwa kwa usahihi kabla ya kuwasilishwa katika maabara kwa ajili ya kuchunguzwa bila kuathiri ubora wake”.alisema Dkt Mboya.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kati, Gerald Meliyo, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba sampuli zinazoletwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali zinakuwa salama ili majibu yapatikane kwa wakati na kwa usahihi ili kutenda haki kwa jamii.

“Tumeleta mafunzo haya muhimu hapa Tabora kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa haki kwa wakati katika nchi yetu. Mafunzo haya yanajumuisha wadau mbalimbali wa haki jinai katika nchi yetu wakiwemo Askari wa Jeshi la Polisi, Madaktari, Waendesha Mashitaka, Mahakimu na Maafisa Ustawi wa Jamii ili waweze kupata na kufahamu vizuri Uchuaji, Utunzaji na usafirishaji wa Sampuli mbalimbali za jinai kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili waweze kutenda haki katika nchi yetu.

Lakini pia na sisi GCLA tuweze kutoa ushauri wa kitaalamu kuwashauri na kupendekeza vitu muhimu vya kuzingatia wakati wa uchukuaji wa sampuli hizo ili kupata sampuli inayojitosheleza na sahihi kwa ajili ya uchunguzi kufanyika na baadae wataalam kwenda kutoa ushahidi Mahakamani na Mahakimu kutenda haki kwa kufuata Ushahidi wa kitaalam wa kisayansi” alisema Meliyo.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatawaongezea ari na umakini mkubwa katika utendaji kazi wao wa kila siku.