Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

DKT. JINGU ATAKA WATAALAM WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA KUWEZESHWA

Imewekwa: 28 May, 2024
DKT. JINGU ATAKA WATAALAM WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA KUWEZESHWA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu ametoa wito kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kuwajengea uwezo wataalam wa tiba asili na tiba mbadala ili waweze kutoa huduma iliyo bora na salama kwa jamii.

Dkt. Jingu ametoa wito huo alipotembelea Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ndogo ya Dar es Salaam Mei 27, 2024 ambapo alitembelea maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba.

Katibu Mkuu amewataka wataalam kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuweza kuwasaidia wataalam wa tiba asili na tiba mbadala na wadau wengine kwani wana imani kubwa na taasisi hii ya Mamlaka.

“Ili wataalam wa tiba asili na tiba mbadala waweze kufanya kazi vizuri ni lazima wafanye kazi na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hivyo ni jukumu letu sote kama wizara na taasisi kuhakikisha wataalam hawa wanawezeshwa kwa kuwapa elimu na kuchunguza bidhaa zao ili waweze kuzalisha kwa ufanisi na kiutaalam bila kuathiri afya za wananchi,” alisema Dkt. Jingu.

Pia, Katibu Mkuu ametoa rai kwa Mamlaka kuhakikisha inasimamia vyema uzalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini zinazotumia kemikali ili kuendelea kulinda usalama wa wananchi lakini pia kuzalisha bidhaa ambazo zitakubalika katika soko la kimataifa kupitia ubora.

Sambamba na hilo, Dkt. Jingu ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri katika mnyororo mzima wa haki jinai nchini kwani Mamlaka inasaidia sana Mamlaka zinazohusika na haki jinai zikiwemo Jeshi la Polisi na Mahakama kwenye kutoa haki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, amemshukuru Katibu Mkuu kwa kutembelea maabara ya Vinasaba na kujionea namna ambavyo uchunguzi wa kimaabara unavyofanyika na pia kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili watalaam wa maabara. Pia, Mkurugenzi amekiri kupokea maagizo ya Katibu Mkuu na kuhakikisha wanayafanyia kazi.