Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

ELIMU ZAIDI YAHITAJIKA KATIKA MATUMIZI YA KEMIKALI

Imewekwa: 25 Nov, 2024
ELIMU ZAIDI YAHITAJIKA KATIKA MATUMIZI YA KEMIKALI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Katabazi, amezitaka Taasisi za Serikali na Binafsi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na matumizi sahihi na salama ya Kemikali.

Kamanda Katabazi amesema hayo Novemba 23, 2024 wakati akihitimisha kikao cha kuhitimisha awamu ya kwanza ya kampeni ya utoaji elimu kwa umma juu ya usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide kilichofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma.

“Kwa upande wa Serikali Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekua ikitoa elimu na mafunzo kwa makundi mbalimbali  ikiwa ni pamoja na wajasiliamali wadogo, wachimbaji dhahabu, wasimamizi wa kemikali  mahala pa kazi, Madereva wanaosafirisha kemikali na jamii kwa ujumla, hivyo niziombe taasisi nyingine za Serikali na Binafsi ziige mfano huo wa GCLA” alisema Kamanda Katabazi.

Akizungumzia lengo la kufanyika kwa Kampeni hiyo ya utoaji elimu kwa umma juu ya usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide ambayo hutumika zaidi kwenye migodi kuchenjua dhahabu, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, amesema kwa kuwa kemikali hiyo inaingia kwa wingi nchini na ni hatarishi hivyo ni vema elimu ikatolewa kwa jamii.

“Tupo hapa kwa kazi maalumu ambayo wadau wanatakiwa kuzingatia kusimamia usafirishaji salama wa kemikali ya Sodium Cyanide, tunafanya hivi cha kwanza kemikali inaingia kwa wingi nchini, cha pili kemikali ni hatarishi kwa maana kwamba ni sumu, na cha tatu kemikali hii inahitajika na ina matumizi makubwa kwenye machimbo ya dhahabu ili tupate dhahabu hivyo ni vema jamii ikaelimishwa” alisema Mkurugenzi Ndiyo.

Naye Msimamizi wa Usafirishaji wa Kampuni ya Uchimbaji wa dhahabu ya Barrick, Joseph Mbanya, amewashukuru wadau wote walioratibu zoezi la kampeni hiyo na kwamba ana imani elimu imeweza kufika kwa wadau na wao kwenda kuelimisha jamii kwa ujumla.