Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MSAJILI WA MAHAKAMA AWATAKA WADAU HAKI JINAI KUSHIRIKIANA

Imewekwa: 03 Feb, 2025
MSAJILI WA MAHAKAMA AWATAKA WADAU HAKI JINAI KUSHIRIKIANA

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, amezitaka taasisi zilizopo kwenye mnyororo wa haki jinai kuendelea kushirikiana ili kutoa haki kwa wakati kwani miongoni mwa nguzo muhimu za mafanikio ni ushirikiano

Nkya ameyasema leo hayo wakati akifunga maonesho ya wiki ya Sheria kitaifa katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, ambapo amezishukuru Taasisi zote zilizoshiriki katika maonesho hayo huku akizitaka kuendeleza ushirikiano huo ili kuongeza ufanisi kwenye upatikanaji wa haki jinai

“Nawashukuru Washiriki wote na wadau wote walioshiriki ninyi ndio chachu ya mafanikio ya wiki ya Sheria ambapo Mahakama tumeshirikiana na wadau wetu kutoa elimu ya Sheria na Haki katika Mabanda na kuwafuata wananchi waliko, na Kupitia kuwafuata wananchi kwenye shughuli zao imesaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi, ikiwa ni kutekeleza mpango wa nguzo ya tatu ya Mahakama ambao unazungumzia kushirikiana na wadau wengine ili kufanikisha kwa ufanisi utoaji elimu ya upatikanaji wa haki” alisema Nkya

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho hayo ambaye ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, amesema maonesho ya mwaka huu yamefanikiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani na nje ya mabanda

“Tulikuwa na Taasisi 39 na jumla ya wananchi 3446 wametembelea mabanda ili kupata elimu ya Sheria haki na utatuzi wa migogoro mbalimbali huku idadi nyingine tumeifikia kwa njia ya vyombo vya habari” alisema George.

Akitoa salam za Shukrani kwa niaba ya Taasisi zote zilizoshiriki katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias, amesema Taasisi zimeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu ya maswala ya haki na kutatua changamoto za wananchi.

“Tumeshiriki maonesho haya kikamilifu tukijikita katika kutoa elimu na kuwahudumia watanzania kupitia miondombinu tuliyowezeshwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kama maono yake yalivyo kuelekea Dira ya Taifa 2050 mifumo isomane kupitia teknolojia na Tehama” alisema Elias.