Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

JAJI KIONGOZI AIPONGEZA GCLA KWA KUTOA MATOKEO YA UCHUNGUZI KWA WAKATI

Imewekwa: 29 Jan, 2025
JAJI KIONGOZI AIPONGEZA GCLA KWA KUTOA MATOKEO YA UCHUNGUZI KWA WAKATI

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa matokeo ya uchunguzi kwa wakati jambo linaloisaidia Mahakama kufikia maamuzi ya mashauri mbalimbali na kufanikisha upatikanaji wa haki kwenye mashauri ya Jinai.

Jaji Kiongozi ameyasema hayo leo alipotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

“Naipongeza sana Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa maboresho makubwa yaliyofanyika na kupelekea kasi ya kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi wa sampuli mbalimbali za makosa ya jinai zinazofanyiwa uchunguzi katika maabara hii, kutoka kwa wakati ni jambo linalosaidia Mahakama kufikia maamuzi ya mashauri mbalimbali na kufanikisha upatikanaji wa haki Jinai” alisema Jaji Siyani.

Jaji Kiongozi Siyani ameongeza kuwa GCLA ina dhamana kubwa kwa wananchi hivyo imani ambayo wananchi na wadau wanayo inapaswa kulindwa kwani kwa sasa kila mtu anaamini matokeo ya uchunguzi uliofanyika na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias, amesema maboresho makubwa ikiwemo ununuzi wa Mitambo ya kisasa uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeleta mapinduzi makubwa na kuongeza kasi ya uchunguzi wa sampuli na kupelekea matokeo kutolewa kwa wakati.

“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya maboresho makubwa kwa kununua mitambo ya kisasa ambayo imeongeza kasi ya uchakataji wa sampuli na kuchochea matokeo kutolewa kwa wakati na kusaidia upatikanaji wa haki” alisema Elias.

Katika hatua nyingine Elias ameongeza kuwa Wataalamu wanaofanya uchunguzi na Maabara zinazofanya uchunguzi zina ithibati za kimataifa.