Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YAPONGEZWA KWA KUWAFIKIA WACHIMBAJI WADOGO

Imewekwa: 10 Feb, 2025
GCLA YAPONGEZWA KWA KUWAFIKIA WACHIMBAJI WADOGO

Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Mhandisi Sabai Nyasili, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kufikisha elimu ya matumizi na utunzaji sahihi na salama wa Kemikali kwa wachimbaji wadogo hasa maeneo ya vijijini ambapo ndio shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu hufanyika.

Mhandisi Nyasili ametoa pongezi hizo Februari 7, 2025 wakati akifunga mafunzo ya matumizi na utunzaji sahihi wa kemikali ya Zebaki kwa wachimbaji wa mgodi wa Sekenke uliopo Shelui mkoani Singida, mafunzo ambayo yaliandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati.

“Tunashukuru sana Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati kwa kuwafikia wadau hawa ambao wao ndio wanatumia Zebaki kila siku ndio wahanga wakubwa, nina amini elimu hii itakuwa msaada mkubwa na kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza wazi juu ya elimu hizi kutolewa mara kwa mara kwa wadau kama hawa” alisema Mhandisi Nyasili

Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Kati, Gerald Mollel, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kemikali ya Zebaki inatumika bila kuleta madhara kwa afya ya binadamu viumbe hai na mazingira.

“Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kemikali ya Zebaki inatumika bila kuleta madhara kwa afya ya binadamu viumbe hai na mazingira kwa sababu kemikali hii inasababisha madhara makubwa pale ambapo haitumiki kwa kufuata maelekezo sahihi, tumesikia ushuhuda hapa wa waathirika wa kemikali kwa hiyo tunaamini baada ya mafunzo haya kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye matumizi” alisema Mollel.

Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo wameishukuru Mamlaka kwa kutoa mafunzo hayo kwani wamekuwa wakitumia kemikali ya Zebaki na wamebaini kwamba wamekuwa wakikiuka baadhi ya miongozo ya matumizi ya kemikali hiyo.

“Ni kweli tunazitaka sana hela lakini afya ndio jambo la kwanza kwangu, mimi mafunzo haya yamenibadilisha nitachukua tahadhari zote ambazo tumefundishwa leo na kiukweli tunamshukuru sana Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutufikia” alisema Aden Daniel.

Kwa upande wa Abdurahman Said amesema baada ya kujifunza madhara ya Zebaki anaiomba Serikali itoe kemikali mbadala ambayo itakuwa na gharama nafuu na haina madhara kama zebaki.