GCLA YASHIRIKI UFUNGUZI WA SIKU YA UFANYAJI MAZOEZI
Watanzania kote nchini wameshauriwa kutenga muda wa kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kila siku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi rasmi wa ufanyaji mazoezi uliiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ufukwe wa Cocobeach,Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt Fidelice Mfumiko amesema utaratibu wa ufanya wa mazoezi hayo utasaidia kulinda afya za wananchi wasipatwe na magonjwa ya kuambukiza.
“Mimi naunga mkono sana uamuzi wa serikali kupitia Mh.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lakini na wito wa Waziri wetu wa Afya, Ummy Mwalimu kwamba tujitokeze kwenye mazoezi haya kama ambavyo yameanzishwa leo katika jiji la Dar es Salaam, Mimi kwa nafasi yangu kama Mkemia Mkuu wa Serikali nasema mazoezi haya yatasaidia sana kulinda afya za wananchi kwa sababu yatatukinga tusipate magonjwa yasiyoambukiza yanayosumbua sana wananchi kama ambavyo yameainishwa,ugonjwa wa kisukari pamoja na shinikizo la juu la damu”.alisema Dkt.Mafumiko.
Dkt Mafumiko pia amewataka watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendeleza utaratibu wa kufanya mazoezi mara wanapomaliza majukumu yao ya kazi ili kulinda afya zao pamoja na kujenga nguvu kazi yanye afya kwa taifa.
“Niendelee kuwakumbusha watumishi wenzangu wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,kama ambavyo sisi tumetoa fursa kwa kufanya mazoezi ofisini, kwa Kanda ya Dodoma na Dar es Salaam tuna gym,basi tuwe tunafanya mazoezi ili tujenge nguvu kazi yenye afya ya mwili, roho na akili”.alisema Dkt Mafumiko.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt Shimo Peter, amesisitiza ufanyaji wa mazoezi wenye kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kula vyakula vyenye afya na kujenga mwili.
“Naishukuru serikali kwa kuruhusu utaratibu huu na kuhamasisha watanzania, lakini pia namshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutenga bajeti ya kufanya mazoezi kila siku. Lakini pia niwashukuru wafanyakazi wenzangu ambao wamekuwa wakifanya mazoezi kila siku kwani tunafahamu mazoezi ni afya ila kitu cha muhimu na kuzingatia ni kwamba ni chakula gani unakula ambacho kinaendana na mazoezi unayofanya,kwa hiyo ukila chakula ambacho ni safi na salama ambacho hakiwezi kujitenga kwenye mwili kitakufanya uweze kuwa na afya njema ambayo itakuwezesha kutenda kazi zako za kila siku bila kupata magonjwa yeyote ya kuambukiza”.alisema Dkt Shimo.
Nae Mkemia kutoka Ofisi ya Kanda ya Mashariki Omary Edward amesema fursa hiyo iliyotolewa na serikali itawanufaisha watumishi kuiwezesha miili yao kuwa imara na kufanya kazi kwa bidii.
“Mimi kama mtumishi pamoja na watumishi wengine utaratibu huu wa ufanyaji mazoezi utatunufaisha kwa kuwezesha miili yetu kuwa imara na kuwa na nguvu ya kufanya kazi” alisema Edward.
Serikali imetangaza rasmi kuwa kuanzia jumamosi ya tarehe 04 Mei,2024 na jumamosi zote zinazofuata kuwa ni siku ya kufanya mazoezi kwa mikoa yote ya Tanzania ili kupunguza kasi ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.