Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YAWAJENGEA UELEWA WAANDISHI WA HABARI JUU YA UDHIBITI WA MADHARA YA SUMU YA MADINI YA RISASI

Imewekwa: 26 Oct, 2023
GCLA YAWAJENGEA UELEWA WAANDISHI WA HABARI JUU YA UDHIBITI WA MADHARA YA SUMU YA MADINI YA RISASI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo chake cha Kudhibiti Matukio ya Sumu imefanya mkutano na Waandishi wa Habari ili kuwajengea uelewa zaidi juu ya Udhibiti wa Madhara yatokanayo na sumu ya madini ya risasi.

Mkutano huo uliofanyika kwa kushirikiana na Asasi isiyo ya kiserikali ya Agenda ulilenga kuwakutanisha wadau wanaohusiana na uzalishaji rangi ambapo ni sehemu moja wapo ya upatikanaji wa sumu ya madini ya risasi na vyombo vya habari.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mratibu wa Kituo cha kuratibu Matukio ya Sumu nchini, Yohana Goshashy, amesema kuwa sumu ya Madini ya risasi yana athari kubwa kwa maisha ya binadamu kwa kuwa yanapelekea mfumo wa fahamu na mfumo wa uzazi kuharibika pamoja na kusababisha ugonjwa wa kupooza.

“Madhara ya madini haya ni makubwa sana lakini uelewa wa wananchi bado sio mkubwa kiasi hicho, ndio maana sisi kama Kituo cha Kuratibu Matukio ya Sumu ambacho kipo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tumeungana na Asasi ya Agenda ili kupeleka msukumo na ujumbe huu kwa wananchi kuweza kujua kwamba kuna matukio yanayohusiana na sumu ya risasi ambayo hatuwezi kuona mara moja madhara yake kwa kuwa sumu hii ni moja ya sumu ambayo madhara yake yanachukuwa muda mrefu kuonekana,” Alisema Goshashy.

Ameongeza kuwa makundi makubwa yanayoathirika kwa kiasi kikubwa ni kundi la akina mama na Watoto. Hata hivyo amebainisha sababu mbalimbali zinazopelekea kuwepo kwa sumu ya madini ya risasi nchini kuwa ni pamoja na matumizi ya bidhaa zenye madini ya risasi ikiwa ni pamoja na midoli ya kuchezea watoto, uchakataji wa betri za magari na ardhi ambayo imeathiriwa inaweza kuwa chanzo kimojawapo cha uzalishaji wa madini ya risasi.

Akisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii, Goshashy amesema kuwa uelewa kwa wananchi bado ni mdogo, hivyo Mamlaka kwa kushirikiana na Asasi za Serikali na zisizo za Serikali imeona ni vyema kutoa elimu kwa vyombo vya habari ambavyo vinaweza kuwafikia wananchi wengi kwa muda mfupi na kwa upana mkubwa.

Kwa upande wake Dorah Swai, Afisa Programu kutoka Agenda, ametoa wito kwa Serikali kuongeza nguvu katika kupiga vita matumizi ya rangi zenye madini ya risasi, ikizingatiwa kuwa kiasi kikubwa cha madhara hayo yapo katika nchi zinazoendelea haswa katika nchi za Afrika, Asia na Amerika ya kusini.