KATIBU MKUU AZINDUA KAMATI YA KITAALAM YA VINASABA VYA BINADAMU
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, ameipongeza Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuunda Kamati ya kitaalamu ya Vinasaba vya Binadamu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Vinasaba vya Binadamu Sura ya 73.
Dkt Jingu ametoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati akizindua Kamati hiyo na kusema kuwa ana imani itasaidia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kutimiza wajibu wake kwa nchi na Serikali na kuendeleza mahusiano mema na Taasisi ambazo zina majukumu yanayoshabihiana.
“Ni matumani yangu kuwa kamati tunayoizindua hii leo itasaidia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kutimiza wajibu wake kwa nchi na Serikali, lakini pia itaendeleza mahusiano mema ya kiutendaji kati ya Mamlaka hii na taasisi ambazo zina majukumu yanayoshabihiana” alisema Dkt Jingu.
Dkt Jingu pia ametoa rai kwa kamati hiyo hasa kwa wanaofanya uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu kufuata maadili ya kazi na kutumia teknolojia za kisasa ili kuepuka madhara au migogoro inayoweza kujitokeza.
“Masuala ya Vinasaba yana mambo mengi ambayo yanaweza kuisaidia jamii, lakini pia yanahitaji kiwango kikubwa cha kimaadili na kiusimamizi, lakini pia ili muweze kufanya kazi vizuri ni muhimu na ni lazima mjihakikishie mnakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya vinasaba duniani kwa kuwa inabadilika kwa haraka sana” alisema Dkt Jingu.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt Fidelice Mafumiko, ametaja majukumu yanayofanywa na Mamlaka ikiwemo sheria ya Udhibiti Matumizi ya Vinasaba vya Binadamu sura ya 73.
“Chini ya sheria hii Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inapata kusajiri na kukagua wadau wa maabara zinazojishughulisha na uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu nchini kwa lengo la kuweza kudhibiti matumizi mabaya ya taarifa za vinasaba, kwa mujibu wa sheria hii Mamlaka pia imepewa jukumu la kutoa vibali vya kufanya utafiti wa suala linalohusisha Vinasaba vya Binadamu” alisema Dkt. Mafumiko.
Nae, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Tumaini Nagu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ameahidi kupokea maelekezo yote yaliyoainishwa kwenye kamati hiyo na kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
“Kwa niaba ya wenzangu wote wajumbe wa kamati hii ya kitaalamu ya vinasaba tunasema tumepokea maelekezo yote, kuhusu unyeti wa kazi hii, lakini pia kuhusu mabadiliko ya teknolojia ambayo yanaenda kwa kasi sana na vilevile maelekezo kuhusu masuala ya ustawi wa jamii na usalama wa watu wenyewe na usalama wa nchi na kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wakati na inazingatiwa. Niseme tu kuwa tumepokea na sisi tunaahidi tutatimiza kazi yetu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo” alisema Dkt. Nagu.