MAAFISA UPELELEZI WASISITIZWA WELEDI KATIKA KAZI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, limewataka wakuu wa Upelelezi pamoja na Askari katika Wilaya zote za Mkoa huo kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, kanuni, sheria na taratibu katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita, Lusajo Mwasalyanda, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Upelelezi juu ya namna bora ya Uchukuaji, Uhifadhi na usafirishaji wa sampuli zinazohusiana na uchunguzi wa Kimaabara wa jinai na sumu yaliyofanyika mkoani Geita Oktoba 24,2024.
“Wito wangu kwa washiriki ni kuyapokea mafunzo haya na kwenda kuyafanyia kazi, lakini kikubwa nawaomba tuzingatie kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, kanuni, sheria na taratibu katika kazi zetu. Katika mafunzo haya tumeita Wakuu wa Upelelezi na askari wa masuala ya jinai, lengo ni kuhakikisha wote tunayapokea vizuri ili tuweze kuwafundisha hata wale walio chini yetu ili kuhakikisha kazi zinafanyika inavyostahili” alisema Mwasalyanda.
Aidha, Mwasalyanda ameipongeza Mamlaka kwa kutoa mafunzo hayo huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo yameleta tija kubwa na kwamba yatakwenda kuwasaidia hata wale walioko chini yao katika utendaji kazi wao.
Kwa upande wake Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa wa Polisi hasa wale wanaohusika na uchukuaji wa sampuli mbalimbali, ikiwemo za Vinasaba, Sampuli za Toksikolojia pamoja na sampuli au vielelezo vya dawa za kulevya, kuhakikisha zinafika maabara zikiwa katika hali yake ya uhalisia na kuwezesha uchunguzi kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
“Tumetoa mafunzo haya ili kuhakikisha kwamba wanavyochukua, wanavyofungasha na wanavyosafirisha sampuli mpaka zinafika maabara zifike na ubora ule ule ili yale majibu wanayotarajia basi waweze kuyapata katika ubora na muda unaotakiwa” alisema Mulima.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kupatiwa elimu hiyo, itawaongezea ufanisi katika utendaji kazi wao na kufanya shughuli ziende kwa weledi zaidi kwa kuzingatia sheria na miongozo ambayo yameelekezwa katika mafunzo.