MAAMUZI YENU YAZINGATIE UAMINIFU, UADILIFU NA WELEDI
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka wajumbe wapya wa Bodi ya Zabuni ya Mamlaka kuzingatia uaminifu, uadilifu na weledi katika utoaji maamuzi katika vikao vya Bodi ya Zabuni.
Mkemia Mkuu wa Serikali amesema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wapya wa Bodi ya Zabuni ya Mamlaka ambayo ameiteua hivi karibuni.
“Natarajia mafunzo haya yatawasaidia kufanya maamuzi kwa spidi na weledi ili kuwezesha utendaji kazi na kuzingatia taratibu za manunuzi. Ununuzi ni zaidi ya kitengo cha ununuzi, mnapaswa kufanya majukumu yenu kwa uaminifu, uadilifu na weledi katika utoaji wa maamuzi bila kukwamisha biashara” alisema.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesihi wajumbe wapya ya Bodi ya Zabuni kuepuka kufanya maamuzi kwa kuangalia mtu mmoja au wachache kati ya wajumbe hao, bali kwa kuzingatia uelewa wa nyaraka zilizwasilishwa kwa ajili ya kufanya maamuzi.
“Tuepuke kufanya maamuzi kwa kuangalia wengine wanasemaje au wameamuaje, tujenge utamaduni wa kusoma nyaraka na kuzielewa ili vikao vya bodi ya zabuni visiwe kwa ajili ya kutoa maamuzi ya haraka au kutoa maamuzi kwa kutegemea mtazamo wa mjumbe mmoja” aliongeza Dkt. Mafumiko.
Vile vile, Mkemia Mkuu wa Serikali, ameitaka Sekretarieti ya Bodi ya Zabuni ya Mamlaka kutimiza wajibu wao wa kutoa miongozo na ushauri inavyopaswa ili kuiwezesha Bodi kufanya ununuzi wenye tija na kimapinduzi kwa taasisi na kuhakikisha thamani ya fedha inafikiwa mara zote.