Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MMS: MWONGOZO UTASAIDIA USIMAMIZI WA KEMIKALI YA AMMONIUM NITRATE

Imewekwa: 25 Apr, 2024
MMS: MWONGOZO UTASAIDIA USIMAMIZI WA KEMIKALI YA AMMONIUM NITRATE

Mwanaheri Jazza

Kutokana na ongezeko kubwa la uingizaji wa kemikali aina ya Amonium Nitrate nchini,Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeandaa mwongozo ili kuweka utaratibu utakaotumika katika usimamizi wa kemikali hiyo katika usafirishaji,Uhifadhi pamoja na utumiaji.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa kemikali cha kujadili rasimu ya mwongozo ya usimamizi wa kemikali hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam,Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt Fidelice Mafumiko, amesema mwongozo huo ni kielelezo cha kuhakikisha uwepo wa biashara endelevu ya kemikali sambamba na kulinda Afya za watu na mazingira.

“Tumeona kwamba kuna umuhimu tunapoona biashara hii ya kemikali ya Amonium Nitrate na kiasi kinachoingia nchini kuwe na mwongozo ambao utasaidia au utaongoza usimamizi wa moja kwa moja kwa wasafirishaji, wahifadhi na watumiaji ili iweze kusaidia katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama katika utumiaji wake”alisema Dkt Mafumiko.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Daniel Ndiyo akizungumzia mwongozo huo amesema kemikali ya Amonium Nitrate inahitaji usimamizi wa hali ya juu hasa katika suala la usafirishaji huku akitolea mfano nchi jirani ya Kenya inavyosafirisha kemikali hiyo kwa kusindikizwa na Jeshi la Polisi.

“Na sisi tutarekebisha katika usafirishaji kwa sababu suala la Amonium Nirate ina sura nyingine kubwa na tofauti katika ulinzi, Kwa mfano nchi ya Kenya usafiri wa Amonium Nitrate inasafirishwa kwa kusindikizwa na Jeshi la Polisi.” alisema Daniel Ndiyo.

Naye mdau wa usafirishaji na mhifadhi wa mizigo kutoka Kampuni ya Fleight Forward Tanzania Ltd, Sadiki Yusuph, amesema mwongozo huo utakwenda kuondoa sintofahamu zote katika utekelezaji na usimamizi salama wa kemikali.

“Mwongozo huu sasa unaenda kuondoa zile sintofahamu zote katika utekelezaji na usimamizi wa kemikali hii ya Amonium Nitrate ambayo ni kemkali muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu.”