MAFUNZO YA USIMAMIZI WA SAMPULI ZA JINAI YAONGEZA TIJA
Wapelelezi na Wachunguzi wa Sampuli ya Sayansi Jinai wameombwa kuzingatia Mafunzo ya usimamizi wa sampuli za jinai yaliyotolewa wataalam kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuongeza Ufanisi na tija katika utendaji wao wa kazi.
Akiongea wakati akifungua Mafunzo ya Utunzaji na Uchukuaji wa Sampuli za Sayansi Jinai kwa jeshi la Polisi ngazi ya Upelelezi, ofisi ya Waendesha Mashtaka, TAKUKURU na Uhamiaji yaliyofanyika Tarime Juni 12, 2026, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mark Njera, amesema kuwa kitu muhimu kwenye maisha ni kuongeza uelewa wa ziada ambao unasaidia katika shughuli za kitaalamu na zisizo za kitaalamu.
“Tukipata fursa ya kujifunza tujibidishe kujifunza ili tuwe na ziada ambayo hatukuwa nayo na kwa kada hii ya wapelelezi na wachunguzi niwaambie jambo moja tu, hakuna ushahidi ambao ukienda mahakamani ni wachache wanaweza kuupima ni ushahidi ambao mtu hawezi kuupinga na uelewa wa kawaida ni ushahidi wakitaalamu, na ukiwa nao uhakika wa kushinda kesi yako ni asilimia nyingi.
Niwaombe tuyazingitie mafunzo haya yatakayotolewa ili yatusaidie kuleta tija, leo tunashindwa kesi mahakamani kwa sababu ya vitu vidogo vidogo ambavyo tungekuwa tunavifanya kitaaalamu mashauri yetu mengi yasingekuwa na vikwazo,”alisema Njera.
Naye Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kimashtaka Tarime, Upendo Malulu, amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuratibu masuala ya upelelezi kwa haki na Usawa pasipo na vikwazo vya kiuchunguzi na kuiomba Mamlaka iendelee kutoa mafunzo mara kwa mara ili kuwajengea uelewa zaidi wapelelezi na wachunguzi wa Sayansi Jinai.
“Mafunzo haya kwetu ni mhimu kufahamu kwasababu tunaratibu upelelezi kwaiyo tumeongezewa mambo mengi sana hususani kwenye eneo la usimamizi wa sampuli za jinai ni eneo mhimu ikizingatiwa kwamba sasahivi ushahidi wa kisanyansi unachukua nafasi kubwa sana kwa kesi nyingi, kwasababu ni ushahidi wa uhakika,” Alisema Malulu.
Aidha Meneja wa Maabara wa Sayansi Jinai Kemia, kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Joyce Njisya, alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwawezesha Maafisa kuchukua sampuli zitakazokuwa na ubora na kumsaidia Mkemia Mkuu wa Serikali kuweza kufanya uchunguzi wa kina na kupata matokeo yatakayokuwa bora zaidi, ambayo majibu hayo yatatumika katika kutoa haki kwa Mahakama za Tanzania.
“Lengo ni kwamba Maafisa Polisi ambao moja kwa moja wanahusika katika matukio ya uchukuaji wa sampuli, waweze kuelewa ni namna gani hizi sampuli zinachuliwa na baada ya kuchukuliwa zinaweza kutunzwa vizuri na kusafirishwa vizuri mpaka maabara zikiwa zimetunza umahili wake ili zisije zikaharibika na katika kutunza umahiri huu lengo kubwa ni kuweza kupata matokeo ambayo ni bora na sahihi kwa ajili ya kutumika katika vyombo vya sheria kama vile Mahakama ili kuweza kutoa haki,” alisema Njisya.
Davis Katesigwa na na Koplo Edgar, Wameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuwaomba wazidi kuwatembelea mara kwa mara kwa ajili ya kutoa elimu kwa sababu mafunzo hayo yanazidi kuwajengea uwezo na uelewa mpana juu ya uchunguzi wa sampuli za Sayansi Jinai.