MAMLAKA IMEPATA MAFANIKIO KATIKA KUPATA ITHIBATI YA MAABARA
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imepata mafanikio katika kupata ithibati ya Maabara zake tano na mbili zilizobaki zitakamilishwa katika mwaka huu wa 2024, kwa kiwango cha kimataifa kwa kiwango cha ISO 17025:2017.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Wakaguzi wa Ndani wa Mifumo ya Ubora katika ukumbi wa Baraza la Uuguzi Ukunga Tanzania kilichopo Kibaha mkoani Pwani Aprili 29, 2024.
Dkt. Mafumiko amesema kuwa Mamlaka imeandaa kikao kazi hicho kwa lengo la utekelezaji wa ithibati ya kiwango cha ISO/IEC 17025:2017 na ISO 9001:2015 ambavyo ni mahsusi katika kuongeza umahiri katika utendaji wa kila siku katika maabara, kuimarisha hadhi ya Maabara za Mamlaka kulingana na viwango na matakwa ya kimataifa pamoja na kuiwezesha Mamlaka kuongeza wigo wa ithibati katika maabara zake.
“Wakaguzi wa ndani ni mhimili muhimu sana ili kuhakikisha kuwa mifumo yetu inakwenda kama inavyotakiwa, hivyo ni muhimu kwa kila mkaguzi kutambua dhamana aliyokabidhiwa kwa ajili ya kutimiza matakwa ya ithibati na kuimarisha utendaji kazi wa Maabara unaozingatia viwango vya kimataifa,” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha, Dkt. Mafumiko amewataka wakaguzi wa ndani kuongeza juhudi kwa kujituma katika kutekeleza, kusimamia na kukagua mifumo ya ubora kulingana na matakwa ya mifumo bora ya maabara ili kulinda ithibati na kuitekeleza kwa vitendo na kuleta sifa nzuri kwa Mamlaka na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora na Usimamizi wa Vihatarishi Benny Mallya, amesema kuwa wakaguzi wa ndani wa mifumo wataendelea kutekeleza majukumu ya ukaguzi kwa umahiri na pia kuhakikisha Mamlaka inatetea na kusimamia vyema ithibati za maabara zilizopatikana.