Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA NA OFISI YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI ZANZIBAR WATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Imewekwa: 20 Aug, 2024
MAMLAKA NA OFISI YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI ZANZIBAR WATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la wawakilishi Zanzibar imetoa wito kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kudumisha na kuimarisha ushirikiano kati yao na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar ili kuhakikisha Taifa linakuwa imara na bora zaidi katika sekta ya Afya.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Agosti 06,2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Sabiha Thani,wakati walipotembelea Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali za kiuchunguzi wa kimaabara zinazofanyika katika Mamlaka hiyo.

“Nitoe wito kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali hapa Bara kuimarisha ushirikiano baina yao na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar katika kubadilishana mawazo, kubadilishana wataalamu ili waende sambamba katika kuhakikisha kuwa Taifa letu linakuwa imara na bora zaidi katika sekta ya Afya. Tunawategemea sana katika kuweka afya za wananchi kuwa bora zaidi lakini pia na vifaa vinavyotumika viwe bora zaidi kwa kuwa Taasisi hizi ni kubwa na zinategemewa sana kwa uchunguzi” alisema Mhe. Sabiha.

Akizungumzia hatua hiyo Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt Fidelice Mafumiko, amesema tayari wamekuwa na ushirikiano mzuri na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar katika masuala ya uchunguzi wa kimaabara lakini ameahidi kuimarisha zaidi ushirikiano huo.

“Tumekuwa tayari tukifanya hivyo lakini tungependa twende  kubadilishana wataalamu wa huku bara waende Zanzibar na wa Zanzibar waje huku bara kwa lengo la kujifunza zaidi, lakini na yale maeneo ambayo tunaona yanaweza kuwa na changamoto tuone kwa pamoja tunayapatia ufumbuzi” alisema Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar, Ussi Kombo, amesema lengo la ujio wao kutembelea Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Mamlaka hiyo ikiwemo kuona Mitambo inavyofanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali hususan katika Maabara ya Sayansi Jinai Toksikojia jambo ambalo litaboresha zaidi utendaji kazi wao katika Maabara zao Zanzibar.