MAMLAKA YAPONGEZWA KWA KUFANYA UCHUNGUZI WA KIMAABARA KWA WAKATI
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepongezwa kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara wa sampuli mbalimbali za makosa ya jinai kwa muda mfupi na kupelekea kukamilisha upelelezi kwa wakati na mashauri kusikilizwa mahakamani kwa wakati.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkoa wa Mtwara Mrakibu Mwandamizi wa Polisi. Adam Salim Amiri, wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Sampuli za Makosa ya Jinai, yaliyofanyika Disemba 16, 2023, Masasi Mtwara yaliyojumuisha maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, Madaktari na Wataalam wa Maabara wanaohusika na mnyororo wa sampuli za makosa ya jinai.
“Napenda kuipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika uchunguzi wa kimaabara wa sampuli mbalimbali za makosa ya jinai na kusaidia kukamilisha upelelezi kwa wakati na mashauri kusikilizwa mahakamani kwa wakati na hivyo kuchangia upatikanaji wa haki kwa wakati”. Alisema Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Amiri.
Aidha, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkoa wa Mtwara, SSP, Amiri, amesisitiza kuwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa uchukuaji wa sampuli au vielelezo na kuviwasilisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa kimaabara ni muhimu, kwa vile upatikanaji wa matokeo sahihi ya uchunguzi wa vielelezo hivyo, huchangiwa kwa kiasi kikubwa na ufanisi wa hatua za awali za uchukuaji wa vilelezo hivyo, ufungashaji na usafirishaji.
Kwa upande mwingine SSP. Amiri amedokeza umuhimu wa uchunguzi wa kisayansi katika ulimwengu wa utandawazi kuwa ndio msingi mkubwa wa kujenga kesi mahakamani.
“Niwaombe washiriki wote wa mafunzo haya kuzingatia mambo mtakayoelekezwa na kwenda kuyafanyia kazi na hatimaye kuleta mabadiliko makubwa katika kusimamia mnyororo mzima wa Haki Jinai kama anavyosisitiza Mheshimiwa Rais wetu”. Alisema.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kusini, Hosea Hosea, amesema kuwa mafunzo hayo yakitumiwa kwa usahihi yatasaidia ukusanyaji wa sampuli, ufungashaji wa sampuli na usafirishaji wa sampuli ulio sahihi ambao utasaidia Mamlaka kufanya uchunguzi na kupata majibu sahihi ambayo mwisho wa siku yatasaidia upelelezi na utoaji wa haki.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Jinai Mkoa wa Lindi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Alton Nelson Mkonyi, akifunga mafunzo hayo amesema kuwa, mafunzo hayo yatakuwa yamefikia mafanikio iwapo washiriki wa mafunzo hayo wataenda kuyatendea kazi yale waliyojifunza na hivyo kutekeleza azma ya vyombo vya Serikali ya kutoa haki kwa watu na kwa wakati.