Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA YATOA VIGEZO VYA UINGIZAJI WA RANGI

Imewekwa: 28 Oct, 2024
MAMLAKA YATOA VIGEZO VYA UINGIZAJI WA RANGI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imezitaka kampuni zinazoingiza rangi nchini na viwanda vinavyozalisha rangi, zatakiwa kuto kuzalisha, kuingiza au kusambaza rangi zenye kemikali ya madini ya risasi ili kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.

Maelekezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo alipokutana na wadau mbalimbali katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya kudhibiti sumu ya madini ya risasi kilichofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 25, 2024.

“Tunapenda mzalishe rangi ambayo haina sumu ya madini ya risasi na endapo mtatumia madini ya risasi, basi iwe kwenye viwango ambavyo vimewekwa kitaifa ili kulinda afya za Watanzania na mazingira na Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa bidhaa zenye madini hayo unadhibitiwa,” alisema Ndiyo.

Aidha, Mkurugenzi alisema kuwa rangi zitakazoingizwa nchini lazima zitachukuliwa sampuli na kufanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha uwepo wa madini ya risasi na kubainisha kama inakidhi viwango na vigezo vya kitaifa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalam ya Kituo cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Profesa Amos Mwakigonja alitoa rai kwa wadau kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mamlaka husika katika kuhakikisha usalama wa nchi unazingatiwa kwa kuzalisha bidhaa ambazo ziko salama kwa matumizi ya binadamu.

Dorah Swai ambaye ni Afisa Programu katika kampuni ya AGENDA, ameipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya kuhakikisha inazuia matumizi mabaya ya sumu ya madini ya risasi na ametoa rai kwa waingizaji, wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa zenye madini ya risasi kuunga mkono juhudi ambazo zipo ili kwa pamoja kulinda usalama wa nchi.