Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MASHAHIDI WATAALAM WAKUMBUSHWA WAJIBU WALIOBEBA

Imewekwa: 14 Jul, 2024
MASHAHIDI WATAALAM WAKUMBUSHWA WAJIBU WALIOBEBA

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka Mashahidi Wataalam kusoma na kujikumbusha mara kwa mara majukumu yao ili kuongeza maarifa zaidi katika kutekeleza wajibu wao.

Dkt. Mafumiko, amesema hayo Julai 12, 2024 Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha Mashahidi Wataalam kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Amesema Mashahidi Wataalam wamebeba wajibu na dhamana kubwa kama watumishi wa Mamlaka ambayo moja ya majukumu yake ni kutoa Ushahidi wa kitaalam mahakamani kwenye mashauri mbalimbali ya jinai.

“Unapotoka kwenda kutoa ushahidi mahakamani, umeibeba Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, umejibeba mwenyewe kama mtumishi wa Umma na umebeba masuala ya Serikali kwa hiyo ni muhimu sana kujua dhamana kubwa uliyobeba”. Amesema

Hata hivyo amewapongeza Mashahidi Wataalam hao kwa kutekeleza wajibu wao vyema wa kwenda kutoa ushahidi mahakamani na hivyo kuweza kufikia asilimia 82 ya kuhudhuria kesi mahakamani  kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024, ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kiwango cha ushiriki wa kesi mahakamani ulikuwa chini ya asilimia hamsini.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Gilbert Ndeoruo, amesema dhumuni la kikao hicho ni  kuondoa changamoto mbalimbali za utoaji ushahidi mahakamani ambapo kulikuwa na ushirikishwaji wa uzoefu wa pande mbili kati ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Maafisa kutoka Ofisi ya Mashtaka, Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani katika kubaini utatuzi wa changamoto hizo.

Naye mmoja wa washiriki wa kikao hicho kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jakson Mwijage, amesema kikao hicho kimekuwa cha manufaa kwao kwa vile wameweza kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika utoaji ushahidi mahakamani na kuchukuliwa kwa ajili ya utatuzi.