Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MIFUMO YA TEHAMA YASAIDIA WADAU KUPATA HUDUMA KWA HARAKA

Imewekwa: 17 Dec, 2024
MIFUMO YA TEHAMA YASAIDIA WADAU KUPATA HUDUMA KWA HARAKA

Kuboreshwa kwa Mifumo ya TEHAMA ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,  hususani ya uombaji vibali vya kemikali, kulipia na kupokea risiti pamoja na kuwasilishwa maoni ya wateja, imetajwa kusaidia na kurahisisha utendaji kazi kwa wadau wa kemikali nchini, kwani kwa sasa  huduma zote unazipata kwa wakati mmoja na muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka hiyo, Sylvester Omary wakati wa mafunzo ya Matumizi salama ya kemikali kwa wasimamizi wa kemikali kutoka makapuni, Taasisi na Mashirika mbalimbali yaliyofanyika Desemba 15, 2024, katika Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha.

Sylvester amesema kimsingi kuboreshwa kwa mifumo hiyo kumerahisisha utendaji kazi katika sekta zote za Mamlaka hiyo, jambo ambalo limewezesha wadau wa kemikali kupata huduma zilizo bora na zenye haraka wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

“Miaka ya nyuma kabla ya maboresho ya mifumo yetu huduma nyingi mlikuwa mkizipata kwa muda mrefu sana, lakini kwa maboresho ambayo yamefanyika siku hizi huduma zetu mnazipata kwa haraka, bila kusahau kupitia mfumo wa E-Mrejesho  mnapewa na fursa ya kuwasilisha maoni yenu na changamoto au pongezi kwa ajili ya kufanyiwa kazi” amesema Sylvester.

Kwa upande wake msimamizi wa kemikali, Rachel Samwel, kutoka kampuni NEELKHANT amekiri uboreshwaji wa mifumo ya maombi ya vibali mbalimbali vya GCLA imewasaidia kuharakisha kupata  huduma mbalimbali ambazo awali iliwalazimu kukaa muda mrefu kuzipata, lakini kwa sasa wanazipata ndani ya muda mfupi.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamehusisha mada mbalimbali kutoka kwa wataalam wa mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo wasimamizi wa kemikali kutoka Makampuni, Taasisi na Mashirika mbalimbali zaidi ya 45 wameweza kushirikia katika mafunzo hayo.